Ukarabati wa mitambo Ubungo IIWataalam wa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa Kushirikiana na Mkandarasi Kampuni ya SIEMENS kutoka nchini Sweden wakiendelea na ukarabati wa mashine  ya Kituo cha Kufua Umeme kwa gesi asilia cha Ubungo II.

Ukarabati huo wa mitambo ulianza Januari 9, 2019 na inatarajiwa kukamilika Februari 13, 2019.

Meneja wa Kituo hicho Mhandisi Lucas Busunge amesema ukarabati huo utahusisha ubadilishaji wa vipuri ili kuiongezea ufanisi mitambo hiyo.

Ameongeza umeme upo wa kutosha, na kusisitiza kuathirika kwa baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar ni  kunatokana na miji hiyo kuchukua umeme kutokea Ubungo ambapo miundombinu yake  haijitoshelezi.

"Kuzimwa kwa mtambo huu tumepunguza Megawati 45, ambazo zinatumika kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar,

"Tungeweza kuchukua umeme kutokea vyanzo vingine vya nje ya Dar es Salaam kuleta Ubungo, hatujafanya hivyo kutokana na aina ya miundombinu iliyopo Ubungo", alisisitiza Mhandisi Busunge.

TANESCO tayari imeshaagiza transfoma kubwa lenye uwezo kwa ajili ya kufungwa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo ili kuondokana na tatizo hilo.

Ukarabati huu unatarajiwa kuongeza ufanisi zaidi katika uendeshaji wa mitambo hii.