kikao na Wahariri Mkoani ArushaMkurugenzi Mtendaji Dkt. Tito Mwinuka amesema ndoto yake kama kiongozi wa TANESCO ni kuona Shirika linajiendesha kwa faida.

Dkt. Mwinuka aliyasema hayo wakati  akijibu swali kwenye kikao cha majumuisho ya ziara ya Wahariri wa vyombo vya Habari waliokuwa wakitembelea miradi wa ukarabati na uimarishaji miundombinu ya umeme, TEDAP, na ule wa Kenya-Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP) TII jijini Arusha.

 Mwandishi alitaka kujua ndoto za Mkurugenzi Mtendaji akiwa ndani ya TANESCO. “Kwanza kabisa huwa nasema hata nikikutana na Wafanyakazi wenzangu kwamba ningependa kuona TANESCO ambayo inafanya kazi kwa faida au ufanisi na ndiko tunakokwenda.” Alisema na kuongeza,

Huu ni mwaka wa pili Shirika letu linaendeshwa bila ruzuku ya Serikali, miaka miwili au mitatu iliyopita ukichukua wastani tulikuwa tunapokea ruzuku ya wastani wa bilioni 200 kwa mwaka, kuna mwaka tulipata 400 na kitu na tukapata 358 lakini hiyo yote sasa hivi haipo tena tunajiendesha bila ya ruzuku ya Serikali. Alibainisha.

Akieleza zaidi, Dkt. Mwinuka alisema huo ndio uelekeo ambao angependa kuushuhudia akiwa TANESCO kwamba Shirika linaendelea kuishi bila ruzuku, Shirika linatengeneza faida na kutoa gawiwo kwa Serikali lakini pia kulipa madeni yote ya nyuma.

“Kwa historia TANESCO tumekuwa na madeni makubwa kutokana na hali mbaya hapo nyuma na madeni haya sasa hayaongezeki, na deni lisiloongezeki ni dalili kwamba tutaanza kulilipa.” Alisema.

Alisema Shirika litaendelea kufanya miradi yake sambamba na kulipa madeni.

Aliongeza katika historia ya nchi hii, Serikaki kupitia TANESCO imeweza kutekeleza miradi mingi mikubwa ya umeme kwa wakati mmoja.

“Katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme kama nguzo ya muhimu ya ujenzi wa Tanzania yenye viwanda, Serikali kupitia TANESCO hivi sasa inatekeleza miradi mikubwa ya umeme 22 kwa wakati mmoja na kwa fedha za Serikali.” Alisema.

Miradi hii inalenga kusogeza miundombinu katika maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme, lakini pia kukarabati miundombinu iliyochakaa au kuzidiwa katika maeneo ambayo yalishafikiwa na umeme.