Lango la kupitishia maji kwenye tunnelShirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kwa Meneja Ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua umeme wa Megawati 2115 kwa njia ya maji wa Julius Nyerere amesema kuwa, kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa handaki la kuchepusha maji katika Mradi huo, kazi inayofuatia hivi sasa ni, uchepushaji wa maji ili kuanza ujenzi wa tuta kuu.

Mhandisi Said Kimbanga amesema kuwa Handaki hilo lina urefu wa mita 703 na upana wa mita 17 huku kimo chake kikiwa mita 12 na zoezi linalofanyika kwa sasa ni utoaji wa udongo kwenye njia ya kuingilia maji, kufikia kwenye level ya mita 68.5 juu ya usawa wa bahari ili maji yaweze kupita.

"Hapa tulipo maji yanapita kuelekea baharini, hatuwezi kujenga tuta kuu hadi tutakapo yachepusha maji kupita kwenye handaki na eneo hilo kubaki kavu" alisema Mhandisi Kimbanga.

Aliongeza kuwa handaki hilo limekamilika kwa asilimia 100, zoezi linaloendelea ni uondoaji wa vifaa ndani ya handaki na kukata udongo uliopo mbele ya lango la kuingilia maji ili kuruhusu maji kuingia ndani ya handaki.

Aidha, kazi nyingine itakalofanyika ni ujazaji wa udongo kwenye mto kujenga tuta (cofferdam) ili kufunga mto na kuruhusu maji kupita kwenye handaki mchepusho.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano TANESCO, Johary Kachwamba amesema kuwa kukamilika kwa mradi wa Julius Nyerere, Tanzania itakuwa na umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.

"Umeme unaozalishwa kwa maji ni umeme wa bei nafuu, kutokana na umeme wa maji kuzalishwa kwa gharama kidogo hivyo tutarajie bei ya umeme kwa Wateja kushuka" amesema Bi. Johary.

Bi. Johary aliongeza kuwa, kutokana na umeme wa maji kuzalishwa kwa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine ambapo unit moja inazalishwa kwa shilingi 36, TANESCO itaweza kujiendesha kwa faida zaidi na kuwezesha umeme wa bei nafuu na uhakika Nchini.

"Tanzania inaelekea sehemu ya kihistoria, kwa kuwa na maendeleo endelevu, tutaokoa mazingira kwani wananchi wataweza kumudu gharama za umeme hivyo kuondoa matumizi ya kuni na mkaa kwa kiwango kikubwa" alisisitiza Kachwamba.