Picha mojaImeelezwa kuwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye uwezo wa  Kilovolti 400 kutoka Iringa hadi mkoani Shinyanga kwa kilomita 670 unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo wakati akiwa katika ziara ya kukagua mradi huo katika mikoa ya  Dodoma, Singida na Shinyanga.
Amefanya ziara katika mradi wa njia ya umeme kv 400 (BackBone Transmission line) unaojengwa kutoka Mkoani Iringa hadi Mkoani Shinyanga ili kuona maendeleo ya mradi huo.

Prof. Muhongo alisema kuwa mradi huo utaboresha upatikanaji wa umeme kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na kaskazini mwa Tanzania ambapo utakuwa na uwezo wa kusafirisha Zaidi ya megawati 2000 kwa wakati mmoja na kwamba gharama za mradi huo ni Dola za Marekani milioni 450.

Alisema kuwa mradi huo pia utafika hadi kwenye mipaka ya nchi za  Tanzania na Kenya, pia katika mpaka wa Tanzania na Zambia ambapo utaiwezesha Tanzania kuuza umeme nchi hizo pale mahitaji ya nishati hiyo yatakapotosheleza nchini.

Awali  Meneja Mradi  wa BackBone,  Mhandisi Khalid James alisema kuwa ujenzi wa mradi huo wa kV 400 umegawanyika katika awamu Tatu ambazo ni Iringa – Dodoma, Dodoma –Singida na Singida- Shinyanga.

Mhandisi James alisema kuwa mradi wa Iringa – Dodoma wenye urefu wa kilometa 225 ambao umekamilika kwa asilimia 100%, unategemewa kuzinduliwa mwezi Septemba, 2016 ambapo mradi huo umefadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 150.

Aidha kwa Laini ya Dodoma – Singida yenye Kilometa 217, alisema kuwa imekamilika kwa asilimia 80% ambapo wafadhili ni Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Japani (JICA) ambao wametoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 169.Mradi huu utazinduliwa Oktoba 2016.

Aliongeza kuwa  laini ya  Singida – Shinyanga yenye Kilometa 228 imekamilika kwa asilimia 99% ambapo mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ulaya EIB (EU) kwa kiasi cha Dola za Marekani  milioni 134 na unatarajiwa kuzinduliwa mwezi Oktoba mwaka huu.

“Mradi huu wa BackBone pia utahusika na uboreshaji wa vituo vya kupooza na kusambaza umeme katika Mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo upanuzi huo unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Korea kwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 36”.

Katika ujenzi huo wa Backbone, Mkandarasi Kampuni ya KEC International ya nchini India inajenga njia za Iringa – Dodoma ambapo kwa upande wa Dodoma- Singida na , Singida –Shinyanga,  Mkandarasi ni Joyti Structures Ltd.

Awamu ya pili ya mradi huu itahusisha kuviongezea uwezo vituo hivyo ili kuweza kuingiza laini mpya ya kV 400 katika mfumo, kuongeza uwezo huko kutahusisha kuweka mitambo ya kupima umeme unaoingia, umeme unaotoka, kulinda laini na zitaongezwa njia za laini kuingia na kutoka.

Katika vituo vya Iringa na Dodoma zimefungwa Transfoma mbili za MVA 250 kilamoja ambazo  zitakuwa zinaingia na kutoka katika vituo hivyo na zitaungwa na laini ya kV 400. Vituo hivyo pia vitafungwa Transfoma mbili kila moja MVA 125 zitakazobaki kwa matumizi ya Mikoa hiyo.

Kwa Mkoa wa Singida zitafungwa Transfoma mbili za kV 250 kila moja kutoka Dodoma na kuelekea Shinyanga, pia itajengwa laini ya kV 400 kuelekea Nairobi itakayopita Namanga Mkoani Arusha mpaka Isanya Nairobi nchini Kenya.

Mkoa wa Shinyanga zitaongezwa Transfoma 2 za MVA 315 kila moja zitakazo tumika migodini na nyingine zitapelekwa Mkoani Mwanza. Transfoma za MVA 125 mbili zitaongezwa kwa matumizi ya Shinyanga.

Images of the event