Naibu Waziri NishatiMradi wa Umeme Vijijini unaotarajia kuunganisha Vijiji vyote vilivyosalia Nchini kufikiwa na Huduma ya Umeme unatarajiwa kuanza rasmi katikati ya Mwezi wa 12 mwaka huu baada ya Wakandarasi watakaohusika na utekelezaji wa mradi huo kuwa wamepatikana na kusainishwa mikataba tayari kwa kuanza kazi mapema.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini Mhe. Dkt Medard Kalemani Mwishoni mwa Juma lililopita akiwa katika Kijiji cha Ulaya kilichopo Wilayani Kilosa alipokuwa akiongea na Wananchi wa eneo hilo katika ziara fupi ya kukagua na maendeleo ya miradi ya huduma za umeme Vijijini Mkoani Morogoro.

“Lengo la Serikali ni kuunganisha Vijiji vyote na Huduma za Nishati ya Umeme kupitia Mradi wa REA III ifikapo Mwaka 2021, Mradi unatarajiwa kuanza Decemba mwaka huu 2016 ambapo maeneo ya Huduma muhimu za Kijamii kama vile Vituo vya Afya, Shule, Pampu za maji zitapewa kipaumbele cha kuunganishwa na Umeme mapema zaidi” alisema Dkt Kalemani.

Aliongeza ya kuwa mradi wa REA Awamu ya III utatekelezwa kwa kutumia nguzo za zege na hivyo kuondoa changamoto za kuungua nguzo na kukatika Umeme mara kwa mara kutokana na matukio ya kuchomwa Nguzo Moto haswa katika maeneo ya Vijijini. Changamoto ambazo zimekuwa zikiigarimu TANESCO fedha nyingi kurudishia nguzo zilizoungua.

Aidha Naibu waziri aliwataka Viongozi na Mameneja wa TANESCO kutenga ofisa mmoja atakayekuwa ni maalumu kwaajili ya kushughulikia miradi ya REA III pekee pamoja na kuhakikisha wanafungua madawati maalumu kwaajili ya kuhudumia wateja huko huko vijijini angalau mara mbili kwa wiki kuondoa changamoto za wakazi wa vijijini kusafiri umbali mrefu kulipia huduma za kuunganishwa Umeme.

Mpango mkakati wa Serikali unaonyesha kuwa, Vijiji 7,673 vitakapelekewa umeme wa gridi katika Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijiji awamu ya Tatu (Turnkey III) utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwaka 2016/17. Mpango huu wa miaka 5 utatekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya Kwanza itatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi 2018/19 (REA IIIa) na Awamu ya Pili itatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Mwaka wa Fedha 2019/20 hadi 2020/21 (REA IIIb).

Kwa mujibu wa taarifa ya maeneo rasmi ya kiserikali kutoka Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tanzania Bara ina jumla ya vijiji 12,259. Kutoka na juhudi za Serikali TANESCO na REA, hadi kufikia Juni 2016 jumla ya vijiji 4,408 sawa na asilimia 36 vimeshafikiwa na umeme. Kati ya Vijiji hivyo, Vijiji 7,673 vitapelekewa umeme wa gridi.
Pia Vijiji 178 vitapelekewa Umeme wa nje ya Gridi kutokana na Nishati jadidifu kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuvipelekea umeme kwa gharama nafuu kwa sasa.