KhalidMRADI wa wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha Umeme (Backbone) ya Msongo wa Kilovolti 400 ambayo inaurefu wa Kilomita 670 kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia Mikoa ya Dodoma na Singida, umekamilika kwa asilimia 100, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi  Khalid Reuben James amewaambia Wahariri wa vyombo vya Habari Mjini Iringa Desemba 19, 2016.


Pia  mradi huo unaohusisha kukamilika kwa upanuzi wa Vituo vinne vya Kupoza na Kusambaza Umeme kwenye Mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga utawezesha kuvipatia Umeme Vijiji takriban 121, vinavyopitiwa na mradi huo, alisema Mhandisi James.


“Mradi huu ni wa muhimu sana kwenye Grid ya taifa kwa sababu utaongeza uwezo wa kusafirisha Umeme kutoka Kanda ya Kusini Magharibi, ambako kuna vyanzo vingi vya Umeme na kupeleka Kanda ya Kaskazini Magharibi na Kanda ya Ziwa ambako kuna shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo Migodi ya Madini.” Alifafanua Mhandisi James.


Kwa mujibu wa Mhandisi huyo, mradi huo ulianza Mwaka 2013, na ulikadiriwa kugharimu kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 470, ambazo zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Wafadhili wakiwemo, Benki ya Dunia, Dola za Kimarekani, Milioni 150, Benki ya Maendeleo ya Afrika, (AfDB),  na Shirika la Maendeleo la Kijapani, (JICA), Dola za Kimarekani Milioni 129.7, Benki ya Uwekezaji ya nchi za Jumuiya ya Ulaya, (EIB), Dola za Kimarekani milioni, 134.5, Shirika la Kiuchumi la Maendeleo ya Korea ya Kusini, (EDCF), Dola za Kimarekani Milioni 36.416, na Serikali ya Norway, Sweden na Tanzania, kupitia kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dola za Kimarekani Milioni 33.4.


“ Ndugu zangu, mradi huu unatoa hakikisho kwa Serikali kuwa mipango yake ya kujenga Uchumi wa Viwanda unawekana pasina shaka, kwani mradi huo mkubwa, utawezesha sasa, kuwapatia Wateja Umeme ulio bora na wa uhakika,” alsiema.
Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari Nchini, wako kwenye ziara ya kutembelea mradi huo ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi mapema Mwaka, 2017.