IssaNA Mwandishi wetu


SHIRIKA la Ummeme Tanzania, (TANESCO), limeeleza chanzo cha kukatika Umeme Januari 24, 2017, ni kulipuka kwa kikata umeme,(Circuit Breaker), baada ya kifaa kijulikanacho kama female Connector ya Umeme wa 132kv kutoka Kituo cha kupoza umeme cha Ubungo kwenda Chalinze kupata hitilafu.


Kwa mujibu wa Meneja Mwandamizi Udhibiti Mifumo ya Umeme TANESCO, Mhandisi Abubakar Issa, alisema hitilafu hiyo ilitokea majira ya Saa 12;32 Asubuhi ilileta athari kwenye mfumo mzima wa GRIDI ya Taifa na kufanya Wateja wa TANESCO walio kwenye Mikoa inayotumia GRIDI ya Taifa kukosa umeme kwa takriban masaa mawili.


Akifafanua Zaidi, Mhandisi Issa alisema, kimsingi mfumo wa GRIDI ya Taifa uko salama na hakuna tatizo lolote, isipokuwa hitilafu hiyo ya kupasuka kwa kifaa hicho kulisababisha mfumo huo kuzima, na umeme ulianza kurejea taratibu kwenye maeneo mbalimbali baada ya tatizo hilo kutatuliwa.


Hata hivyo alisema kifaa kilichoharibika kinasafirishwa kutoka Mkoani Tanga, na mara kitakapowasili kitafungwa na hivyo kurudisha hali ya upatikanaji umeme kwenye eneo lililoathirika Chalinze kurejea kama ilivyo kawaida.
Jitihada za kurejesha Umeme zilifanyika mara tu baada ya hitilafu kutokea na maeneo yote yaliyounganishwa katika GRIDI ya Taifa yalipata umeme.