5R5A3713KAIMU Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt.Tito E. Mwinuka, amefanya ziara ya kutembelea Vituo vitatu vya Kupoza na Kusambaza Umeme vya Mbagala, Kurasini Wilayani Temeke na Kariakoo Wilayani Ilala jijini Dar es Salaam Februari 4, 2016.

Katika ziara hiyo Dkt. Mwinuka aliambayo aliambatana na Waandishi wa Habari na kuwaomba kufikisha ujumbe kwa Wateja wa TANESCO, kwa kuwataka kuwa wavumilivu wakati juhudi za kukamilisha Miradi ya uboreshaji Umeme ikiwa inakaribia kukamilika.

Dkt. Mwinuka alisema,  ongezeko la Watu na shughuli za Kiuchumi maeneo ya Mbagala, Kigamboni na Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, kumepelekea upatikanaji wa umeme kwenye maeneo hayo kuwa na matatizo kidogo kwani vituo vinavyosambaza umeme kwenye maeneo hayo vilikuwa na ukubwa wa kupoza na Kusambaza umeme wa Kilovoti 33 tu, na ndio maana Serikali kupitia TANESCO inaviborehsa vituo hvyo vya Kupoza na Kusambaza Umeme kwa kuviongezea uwezo mkubwa  wa Kilovoti 132.

“Barabara zinapozidiwa na magari ni rahisi sana kubaini kutokana na ongezeko la magari yanayotumia barabara hizo, lakini ongezeko la watumiaji umeme na shughuli za kiuchumi inakuwa vigumu kubaini kwa haraka, kwa hivyo niwaombe Wateja wetu kuwa wavumilivu kwani tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi katika kipindi kifupi kijacho.” Alisema Dkt. Mwinuka.

Dkt. Mwinuka pia alibainisha, kuwa kazi ya kuongeza ukubwa wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme inaendelea kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi ambako nako vituo vya sasa vya ukubwa wa Kilovoti 33, vinabadilishwa na kuwa na uwezo wa Kilovolti 132.
 
Aidha amewapongeza Wakandarasi kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa haraka ili kuwaondolea adha Wateja kwa umeme ulio bora na wa uhakika.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke Mhandisi Jahulula Maendeleo alisema Kituo cha Mbagala kinapata umeme wa msongo wa Kilovolti 33 kutoka Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Ilala kupitia Kurasini.

“Kuna njia ya umeme nyingine ya 33 kV kutoka Kipawa inapita kwa wateja wakubwa, hadi Tandika, Mkulanga na Kongowe, na kuna njia nyingine ya 33 kV kutoka Kipawa kupitia Chang’ombe hadi Kigamboni”. Alisema Mhandisi Maendeleo.

Aliongeza kukamilika kwa Miradi hii katika vituo vya Mbagala na Kurasini kutaondoa tatizo la umeme kuwa mdogo na kukatika katika kwa umeme hasa maeneo ya Kigamboni.