Kombe Wahandisi WanawakeKaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka, amewataka Wahandisi Wanawake wa TANESCO, kutembelea mashuleni ili kuwahamasisha (Motivate), wanafunzi wa kike wapende kujisomea masomo ya Sayansi na Hisabati na hatimaye baadae waje kushika nafasi kama walizonazo wao.


Dkt. Mwinuka aliyasema hayo Makao Makuu ya TANESCO jijini Dar es Salaam, wakati akiwapongeza Wahandisi Wanawake baada ya kupewa tuzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuibuka na ushindi wa kwanza katika Kongamano la Wahandisi Wanawake Tanzania “Tanzania Women Engineers Convention and Exhibition, (TAWECE), ambalo huenda sambamba na maonesho ya shughuli za kihandisi lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.


“Niwapongeze sana kwa kuibuka washindi wa kwanza kwenye maonesho hayo, lakini niwaase, mpatapo nafasi mtembelee mashuleni ili muwahamasishe Wanafunzi wa kike kupenda kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati, na kwa kupitia kwenu, wanaweza kujitokeza wasichana wengi kupenda masomo hayo na hivyo baadaye kufanya kazi za kihandisi kama nyinyi.” Alisema Dkt. Mwinuka.
Dkt. Mwinuka alisema, tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa TANESCO kwani inajenga picha (image) nzuri mbele ya jamii kuonyesha juhudi zetu za kuwahudumia Wateja. Aliongeza.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake kwenye hafla hiyo fupi, Mhandisi Rosamystica Luteganya, alisema Wahandisi Wanawake kutoka TANESCO, walionyesha umahiri wao katika kuelezea teknolojia ya usimamizi wa miundombinu ya usambazaji umeme (Distribution Control Centre), inayotumia kuboresha huduma wanazozitoa katika jamii.


“Lakini pia si hivyo tu, tulionyesha uboreshaji wa huduma tunazozitoa kwa Wateja kwa kutumia Teknolojia ya kisasa kupitia mfumo wa fiber ambao hupitisha taarifa mbalimbali kama vile mawasiliano na picha na hii inawezesha mfumo kuliona tatizo la mteja mara tu linapotokea na
kuwezesha TANESCO kuchukua hatua haraka bila mteja kupata usumbufu.” Alisema Mhandisi Luteganya.


Katika Kongamano hilo la Mwaka huu lililofanyika Julai 29, 2017, kulikuwa na makundi matatu ya washiriki, ambayo ni Shule za Sekondari, Taasisi za Elimu ya Juu na Mashirika ya Umma ambapo waandaaji waliangalia uandaaji, uelewa wa washiriki pamoja na teknolojia ilivyotumika.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji na Huduma kwa Wateja, Bi. Joyce Ngahyoma, alisema ni wajibu wa wanawake kujiamini katika utekelezaji wa majukumu yao na kuachana na dhana ya woga.


“Fanyeni kazi kwa bidii na maarifa, na niwaambie, utendaji kazi wako ndio utakaopelekea kukupandishwa cheo na sio jambo lingine lolote lile, mimi nitastaafu hivi karibuni, ninawaeleza haya kwavile ninajua umuhimu wa kujituma katika kazi na kujiamini.” Alisema Bi.Ngahyoma.
Alionesha kufurahishwa kwake, na angependa idadi ya Wanawake viongozi ndani ya TANESCO inaongezeka na kufikia sio asilimia 50 tu bali asilimia 75 au zaidi.