Ziara ya Naibu WaziriSERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), imeahidi kusimamia miradi ya umeme Kituo cha Tipper-Kigamboni,  Mbagala na Kurasini ili kuhakikisha inakamilika kwa haraka na kwa wakati na hatimaye Wananchi wa maeneo hayo wanaondokana na adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, mwishoni mwa ziara yake ya kufuatilia uboreshaji wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha kufua na kusambaza umeme huko Kimbiji  Wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Waziri pia amekagua ujenzi wa mradi wa maendeleo ya upanuzi na upatikanaji nishati (TEDAP), wa kusafirisha umeme wa 132kv ulioko Gongolamboto nje kidogo ya Jiji.

“Wananchi wanataka umeme, hawahitaji kujua  nguzo za umeme zimepatikana wapi, au upembuzi yakinifu utakamilika lini, nimeagiza baada ya siku tano, fanyeni kazi usiku na mchana walau vituo viwili vya kupoza na kusambaza umeme viwe vimekamilika ili Wananchi wa Mbagala na Kigamboni wapate umeme wa kutosha.” Alisema Dkt. Kalemani mbele ya Mbunge wa Kigamboni Dkt. Faustine Ndungulile, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Hashim Mgandila na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi, Dkt. Tito Mwinuka na viongizi wengine wa TANESCO.

Dkt. Kalemani alisema, Miradi hiyo imechukua muda mrefu, na kwamba hakuna muda zaidi utakaoongezwa kuikamilisha.

Serikali kupitia TANESCO, inatekeleza miradi mitano ya kuongeza kiasi cha umeme kwenye maeneo ya Mbagala na maeeno kadhaa ya wilaya ya Temeke, Kurasini na Kigamboni ili kukabiliana na ongezeko la kasi la watu na shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.

Aidha, Naibu Waziri aliipongeza TANESCO, kwa kutekeleza agizo lake la kuhakikisha wakazi 3,500 wa Kigamboni waliolipia ili kuunganishiwa umeme, wawe wameunganishiwa ifikapo Septemba 15, 2017 ikiwa ni pamoja na kupeleka nguzo za umeme zaidi ya 1,000 maagizo ambayo yametekelezwa.

Hata hivyo Naibu Waziri alimueleza Mheshimiwa Mbunge wa Kigamboni na Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa tiba mahsusi ya upungufu wa umeme kwenye wilaya hiyo ni kukamilika kwa ujenzi wa kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme cha Kimbiji.

“Tiba kubwa ya matatizo ya umeme kwa watu wa Kigamboni, na Mbagala ni hapa Kimbiji(kituo kipya), vile vituo vingine vitapunguza tu matatizo lakini naomba Mheshimiwa Mbunge, uwafikishie ujumbe wananchi kuwa Serikali ya awamu ya Tano inayo dhamira ya kweli ya kuhakikisha inawapatia umeme wa uhakika sio tu wananchi wa Kigamboni bali watanzania wote kwa ujumla.” Alifafanua Dkt. Kalemani.

Naibu Waziri ameshuhudia hatua mbalimbali za ukamilishaji wa miradi hiyo zikiwa zimefikiwa ambapo katika kituo maeneo yote aliyotembelea.

Kuhusu ujenzi wa kituo kipya cha Kimbiji, Dkt. Kalemani amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANSCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, kuwaleta mafundi wa TANESCO wealiotekeleza kwa muda mfupi ujenzi wa mradi wa kituo cha kupoza na ksuambaza umeme kule Mtwara ili waje kuongeza nguvu.