Ziara ya Naibu Waziri Mkoa wa IlalaNa Henry Kilasila

Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Matogolo Kalemani, amekagua Miradi ya uboreshaji wa Miundombini ya Umeme Jijini Dar es Salaam, inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kukagua vituo vya kupoza na kusambaza umeme vya Ilala, City Center, Muhimbili, Masaki na Msasani iwapo vimekamilika na vinafanya kazi vizuri, ambapo aliridhishwa na vituo hivyo.

Aidha, Dkt. Kalemani aliipongeza Menejimenti ya TANESCO, Uongozi wa Kanda, Mkoa na Wafanyakazi kwa kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo, Chuo cha Muhimbili na Hospitali ya Mwananyamala ambapo kila moja imejengewa njia ya umeme ya msongo wa Kilovolti 11 hivyo kuondoa matatizo ya umeme katika maeneo hayo.

“Mahitaji ya Muhimbili ni Megawati 4 wakati kituo cha Muhimbili kinamegawati 12, mahitaji ya Hospitali ya Mwananyamala ni Megawati 1.5 wakati kituo kina Megawati 12, hivyo sitegemei kusikia umeme umekatika katika maeneo haya”. Alisema Dkt. Kalemani na kuutaka Uongozi wa TANESCO kuvisimamia vizuri vituo hivyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugrnzi Mtendaji TANESCO Dkt. Tito E. Mwinuka alisema, Serikali iliona uwepo mkubwa wa mahitaji ya umeme, hivyo kupitia TANESCO iliamua kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na kuviongezea uwezo Vituo vya kupoza na kusambaza umeme, uboreshaji wa vyumba vya kuendeshea mitambo pamoja na uboreshaji wa njia za kusafirisha umeme.

“TANESCO tunafanya jitihada za kuendelea kukamilisha Miradi ambayo haijakamilika ya Mbagala na Kurasini, kwani Miradi hiyo ikikamilika maeneo ya Kigamboni yatapata umeme wa uhakika hivyo mji wote wa Dar es Salaam kuwa na umeme wa uhakika.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri pia alitembelea Chuo cha Ufundi TANESCO cha Masaki eneo ambalo Wanafunzi wanafanya Mafunzo kwa vitendo na kutoa pongezi kwa TANESCO na kuutaka Uongozi kuongeza idadi ya Wanachuo.

Serikali kupitia TANESCO imeendelea na uboreshaji wa Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam ambapo kwa Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ilala kimeongezwa uwezo kutoka MVA 210 hadi MVA 240, ujenzi wa chumba kipya cha kuongezea mitambo na kujenga njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 132 kutoka Ubungo hadi Ilala.

Pia ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme kupitia chini ya ardhi ya msongo wa Kilovolti 33 katika Vituo vya City Center, Sokoine, Railway na Kariakoo.