Uzinduzi wa Ofisi Mkoa wa KilimanjaroKatika kutekeleza agizo la Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, TANESCO imesogeza huduma karibu zaidi na Wananchi ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za TANESCO.


Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alipokuwa akizindua miradi ya umeme Vijijini aliitaka TANESCO kusogeza huduma jirani na Wateja ili kuwarahisishia na kuwaondolea adha Wateja.


Mkoa wa Kilimanjaro umetekeleza kwa vitendo agizo hilo la Mheshimiwa Waziri kwa kufungua Ofisi ndogo tatu katika Wilaya za Same na Mwanga siku ya Ijumaa ya Octoba 13, 2017.


Ofisi hizo zimefunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe. Rosemary Senyamuli, na kuipongeza TANESCO kwa hatua ambazo imefikia.


Ofisi hizo zimefunguliwa maeneo ya Hedaru inayotarajiwa kuhudumia wakazi 10,000 ambapo awali iliwalazimu kutembea Kilometa 54 hadi Same kupata huduma, Kisiwani wakazi 4000 ambapo awali iliwalazimu kutembea Kilometa 25 hadi Same kupata huduma, na Spillway / Nyumba ya Mungu Wakazi 4000 pia iliwalazimu kutembea Kilometa 38 kufuata huduma.


Aidha, katika tukio hilo Wateja walipatiwa elimu ya Usalama kwa kujihadhari na ajali za umeme.


Mteja wa kwanza kuhudumiwa katika Ofisi ya Hedaru Bw. Issa Mshana ameishukuru TANESCO kwa kufungua Ofisi jirani na makazi yao jambo litakalo harakisha huduma na kuwapunguzia gharama za kufuata huduma.