raisAkizindua Mradi wa kufua umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi II Megawati 240 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliwashukuru Wafanyakazi wa TANESCO kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali.

“Mnahangaika kwa kweli kwa kazi nzuri, na mimi nafikiri Mheshimiwa Waziri na Bodi ya Wakurugenzi kama mkipata mabakibaki ya kuwaongeza mshahara msisite, mimi sina tatizo na Wafanyakazi hawa wanafanya kazi nzuri”. Alisema Mhe. Rais.

Akijibu ombi la Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Tito E. Mwinuka la Serikali kuipunguzia tozo TANESCO, alisema kumekuwa na malalamiko mengi kati ya Taasisi za Serikali na kuzitaka kufanya kazi pamoja na kushirikiana hasa wakati wa utekelezaji wa miradi mikubwa.

Aliongeza, kwa sasa mahitaji ya nchi ni Megawati 1, 400 na uzalishaji unafikia Megawati 1,515.3  na kusisitiza bado Tanzania inahitaji umeme wa kutosha.

“Kupatikana kwa umeme wa kutosha ndiko kutakaofanikisha Tanzania ya Viwanda”. Alisema Mhe. Rais.

Mradi wa Kinyerezi II Megawati 240 ulibuniwa ili kuongeza uwezo wa kufua umeme kutokana na gesi asilia na hivyo kuimarisha na kuongeza uwezo wa gridi ya Taifa katika kusafirisha na kusambaza umeme nchini.

Mradi huu unahusu ununuzi, usanifu, utengenezaji wa mitambo na viambata vyake, usafirishaji, ujenzi na ufungaji wa mitambo, ujenzi wa miundo mbinu ya ndani na nje ya kituo (k.m. barabara n.k.), ujenzi wa kituo cha kupokea na kupozea umeme (Substation) pamoja na ukamilishaji na ukabidhi wa mitambo ya kufua umeme.

Aidha, kituo cha Kinyerezi II ni teknolojia mpya na ya kwanza kufungwa nchini ambapo ina hatua mbili ya kufua umeme (Combined cycle).

Mkandarasi wa mradi ambaye ni Sumitomo Corporation kutoka Japan alianza kazi tarehe 1 Machi 2016.

Gharama za mradi ni dola za Marekani milioni 344. Gharama hii haihusishi kodi mbalimbali kama vile Gharama za njia ya reli na bandari, tozo ya mizigo mizito inayotozwa na TANROADS na VAT. Mpaka sasa gharama ya mradi imefikia dola za Marekani milioni 356.2.

Pia, unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa njia ya mkopo kutoka Benki ya Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC) na Japan Bank for International Cooperation (JBIC) za Japani Chini ya mpango wa mikopo ya masharti nafuu kwa asilimia 85% sawa na Dola za Marekani milioni 292.4 na pia mchango wa Serikali ya Tanzania kwa asilimia 15% sawa na Dola za Marekani milioni 51.60.  Mkataba wa mkopo huu ulisainiwa Machi 2015.

Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshalipa fedha yote inayohitajika yaani asilimia 15% ya fedha za mradi kiasi cha Dola za Marekani milioni 51.60. 

Hadi kufikia mwisho wa mwezi February 2018 malipo ya kiasi cha dola za Marekani milioni 258.8 kwa kazi zinazoendelea yameshafanyika kutoka kwenye kiasi cha dola za Marekani milioni 292.4(mkopo wa masharti nafuu wa 85%) ambayo ni sawa na asilimia 88.5.