WebWaziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amefungua mafunzo ya siku Tano ya wasimamizi wa mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) yanayohusisha wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) yanayolenga kuboresha utekelezaji wa mradi huo.


Mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Mipango jijini Dodoma yamehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Michael Nyagoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.


Akifungua mafunzo hayo, Dkt Kalemani ametoa maagizo mbalimbali ikiwemo; wakandarasi wa umeme vijijini mara wanapomaliza kazi za usambazaji, wanapaswa kukabidhi mradi huo kwa TANESCO na REA kabla ya kuondoka katika eneo husika ili kama kuna mapungufu, yarekebishwe kabla ya makabidhiano rasmi.


Pia amewaagiza wasimamizi wa mradi huo, kuruhusu wananchi kulipia kidogo kidogo malipo ya uunganishaji wa umeme na wanapokamilisha malipo hayo waunganishiwe umeme ndani ya Siku Saba.


Vilevile ameagiza wasimamizi wa mradi wa REA III kutoka Wizara, TANESCO na REA kuhakikisha kuwa, wanakuwepo katika eneo la mradi ili kusimamia wakandarasi na hivyo kuongeza kasi na ufanisi katika utekelezaji.


Aidha amegiza kuwa, Taasisi za Serikali zinazohusika na utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kama vile Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, zishirikishwe katika hatua mbalimbali za utekelezaji ili kutochelewesha utekelezaji wake.


Vilevile amewataka Mameneja wa TANESCO, kuanzisha kwa vituo vya kuhudumia wananchi katika kila eneo nchini ili kuepusha wananchi hao kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa katika kutafuta huduma zinazotolewa na TANESCO.


Dkt. Kalemani pia amewakumbusha watendaji wa TANESCO na REA kuhakikisha kuwa, wananunua vifaa vinavyozalishwa hapa nchini vya usafirishaji na usambazaji wa umeme kama nguzo, transfoma na mita za umeme kwani vinatosheleza mahitaji.


Maagizo mengine yaliyotolewa ni pamoja na Ofisi za TANESCO za Wilaya kuwa na stoo ya kuhifadhi vifaa vya umeme, kuhakikisha kuwa kanuni za manunuzi hazicheleweshi utekelezaji wa mradi na wataalam hao kuhakikisha kuwa hawachelewi katika kushughulikia majalada yanayohusu miradi ya umeme.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, alisema kuwa, maagizo ya Waziri ikiwemo suala la ufanyaji kazi kwa kasi, ufasaha na tija yatazingatiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.


Aliongeza kuwa, Bodi ya Shirika hilo haitawavumilia Watendaji watakaopokea miradi kutoka kwa wakandarasi ikiwa na mapungufu na hivyo kuharibika ndani ya muda mfupi.