Waziri kikao cha wadau NjombeWaziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema katika kuelekea uchumi wa viwanda nchi inahitaji umeme mwingi, wa uhakika, gharama nafuu na unaotabirika.

Ameyasema hayo Mkoani Njombe katika kikao kilichoshirikisha wadau mbalimbali wa ujenzi Miradi wa Maporomoko ya maji mto Rufiji (Rufiji Hydropower Project).

Alisema mradi huo ni wa miaka mingi, ulianza kubuniwa tangu Serikali ya Awamu ya kwanza mwanzoni mwa miaka ya sabini.

"Leo tunautekeleza takribani zaidi ya miaka arobaini, lakini ni kweli wakati ule mahitaji yetu ya umeme yalikuwa madogo sana na idadi ya Watanzania ilikuwa haijafika hata milioni arobaini,

"Lakini leo mahitaji yetu ya umeme ni makubwa mno na tunataka kujenga Tanzania ya Viwanda hivyo Serikali imeamua kutekeleza mradi huo", alisema Dkt. Kalemani.

Aliongeza, kwa sasa tuna umeme wa kutosha lakini hauwezi kutosheleza mahitaji ya miaka ijayo kwenye kujenga uchumi wa viwanda.

Alisisitiza kuwa, TANESCO inatakiwa kuzalisha umeme wa kutosha, wa uhakika na unaotabirika lakini pia wa bei nafuu na hivyo utekelezaji wa mradi huu ni muhimu sana.

"Potential ya maji tuliyonayo sasa hivi Tanzania ni maji ambayo yanaweza kuzalisha zaidi ya MW 4700 uwezo tulionao na ambao hatujautumia", alisema.

Aidha, Serikali itaendelea kuzalisha umeme kupitia vyanzo tofauti ikiwemo makaa ya mawe, gesi, joto radhi, upepo na mingine mingi.

Chanzo kikubwa cha maji katika mradi wa Maporomoko ya mto Rufiji ni Mto Kilombero, Ruaha Mkuu na Mto Wegwe.

Ambapo mito hiyo inapata maji kutoka vyanzo vya maji vya nyanda za juu kusini hususani maeneo ya Njombe, Makete na Waging'ombe.