Website KilimanjaroSHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeungana na Watanzania katika kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kupanda miti elfu kumi (10,000) mkoani Kilimanjaro.
Sambamba na upandaji huo wa miti, TANESCO pia imetoa elimu ya uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kutunza miundombinu ya umeme ambayo imekuwa ikiathiriwa mara kwa mara na  miti inayopandwa jirani na miundombinu.
Kampeni hiyo ya upandaji miti ilizinduliwa rasmi Oktoba 14, 2018.na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Kippi Warioba ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi katika shule ya Msingi Muungano katika Manispaa ya Mji wa Moshi.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo ya kupanda miti, Mhe.Warioba aliipongeza TANESCO  kwa jitihada zake za dhati za kuungana na wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro katika kutunza mazingira kwa kupanda miti katika wilaya za Moshi, Rombo, Same, Mwanga, Hai na Siha lakini pia kuelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti.  
Aidha Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa, aliitaka TANESCO kuendelea kutoa elimu ya upandaji miti ili wananchi waelewe maeneo sahihi ya kupanda miti bila kuathiri miundombinu ya umeme.
 “Ni wajibu wa kila mwananchi kujenga utamaduni wa kutunza mazingira, kwa kupanda miti hususan ya matunda, kwani utafaidi kivutli, matunda na wakati huo huo unakuwa umetunza mazingira.” Aliasa Mhe. Kipi Warioba.
Kwa upande wake Menja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro. Mhandisi Mahawa Mkaka akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka alisema kuwa zoezi hilo linalengo la kuelimisha wananchi maeneo  sahihi ya kupanda miti ambayo hayaingiliani na miundombinu ya umeme ili kuepusha madhara mbalimbali kama vile ajali za umeme na upotevu wa umeme pia na uhifadhi wa mazingira.
Mhandisi Mkaka alisema TANESCO ina misongo mbalimbali ya umeme hivyo wananchi wanapaswa kuzingatia sheria inayotaka shughuli za kijamii ikiwemo upandaji wa miti zifanyike umbali wa mita mbili na nusu kutoka kwenye miundombinu ya umeme hii itapunguzi tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Zoezi hil la upandaji miti lilifanywa na wafanyakazi wa TANESCO Mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na Mbunge wa viti maalum Bi. Ester Mmasi anae wakilisha Vyuo Vikuu na Naibu Meya Manispa ya Moshi Mhe. Jomba Koyi.
TANESSCO inategemea kutekeleza zoezi hili la upandaji miti nchi zima ili kuhakikisha jamii inapata elimu ya jinsi ya upandaji miti na pia utunzaji wa miundombinu ya umeme, alisema Mhandisi Mkaka kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka.