Renata bagamoyoShirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeazimia kwa pamoja kuendelea kujipanga kuboresha na kuimarisha zaidi shuguli za ugavi pamoja na manunuzi kupitia kikao kazi cha viongozi waandamizi wa Shirika, wadau pamoja na maofisa ugavi na Ununuzi kutoka ofisi mbalimbali za TANESCO Nchi nzima.

Hayo yamebainishwa na Afisa Fedha Mkuu wa TANESCO Bi. Renata Ndege alipokuwa akifungua kikao kazi hicho cha siku mbili kwa maafisa ununuzi na ugavi wapatao takriban 220 kutoka ofisi mbalimbali za TANESCO Nchi nzima. kikao kinachofanyika kuanzia Novemba 15 mpaka 16 jijini Dar es salaam.

“Tutakapoboresha shughuli za manunuzi na stoo hata shughuli zetu zitakwenda kwa ufanisi na uharaka zaidi hivyo kuongeza tija katika utendaji kazi utakaoliwezesha shirika kufikia malengo yake kwa haraka zaidi. Kupitia kikao cha leo tutafundisha, tutajadiliana pamoja kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kuelekea utoaji huduma bora za ugavi na manunuzi kwa shirika letu na wateja kwa ujumla” alisema Bi. Renata

Aliongeza kuwa, kwa mwaka 2016/17 Shirika lilifanya vizuri kwenye mahesabu na kupata hati safi ya ukaguzi, lakini upande wa ugavi na hasa stoo za Shirika
ni maeneo ambayo bado jitihada kubwa zinahitajika ili kurahisi na kuharakisha utendaji kazi wa Shirika wenye ufanisi lakini pia katika mazingira salama bila kulisababishia shirika hasara ya upotevu wa vifaa na thamani mbalimbali

Ni lazima stoo zetu zote ziwe na vitendea kazi vyote vinavyotakiwa kama vile Kompyuta pamoja na mazingira rafiki ya kufanyia kazi kwa wafanyakazi, na kila vifaa vinapotoka ama kuingia ni vyema vikarekodiwa vizuri kwenye mifumo yetu bila kukosea kwani vifaa vyetu vingi vinapatikana kwenye mifumo hiyo’’ aliongeza Bi. Renata

Aliendelea kwa kuelekeza mameneja waandamizi wa TANESCO ngazi ya kanda kuhakikisha wanasimamia na kuratibu kwa ukaribu maboresho hayo ya stoo za shirika na shughuli za ugavi zinazofanyika ngazi za kanda mpaka wilaya. Pia alisisitiza kwa vifaa vibovu ama vile ambavyo havina matumizi tena ndani ya shirika ni vyema taratibu na kanuni za shirika zikafuatwa vifaa hivyo vikatolewa ama kupigwa mnada na hivyo Stoo zote za shirika zibaki safi na kuwezesha utunzaji na utoaji mzuri wa vifaa kwa shughuli za Shirika.