Ikulu uwekaji sainiRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri Mkuu wa Misri Dkt. Mostafa Madbouly wameshuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi Mradi wa kuzalisha Umeme wa Rufiji (RHPP) Megawati 2100 kati ya TANESCO na Kampuni ya Arab Contractors ya nchini Misri.

Sherehe za kusaini zilifanyikaDisemba 12, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam mbele ya viongozi Wakuu wote wa Serikali, viongozi wa dini na ujumbe kutoka nchini Misri ukiongozwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Mheshimiwa Rais alisema mradi huo ulianza tangu enzi za hayati Baba wa Taifa Mwalimu J.K Nyerere miaka ya 70, ambapo upembuzi yakinifu ulifanyika kati ya mwaka 1976 na 1980.

"Leo tunaposaini mkataba huu ni zaidi ya miaka arobaini, tunautekeleza kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha shilingi Tirioni 6.558" alisema Dkt. Magufuli.

Aliongeza Serikali umeamua kuutekeleza mradi huo kutokana gharama za utekelezaji mradi wa maji ni nafuu na unatija kwa Taifa.

"Ndugu zangu gharama ya kuzalisha unit moja kwa kutumia maji ni senti 36, ni nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine", alisema.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema wakati wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu J.K Nyerere mradi haukutekelezwa kutokana na mahitaji ya umeme kipindi hicho hayakuzidi Megawati 100.

Sababu nyingine hali ya uchumi ulikuwa hairidhishi.

Akielezea hatua za ujenzi alisema mradi utaanza kwa kujenga kuta mbili kubwa, ujenzi wa bwawa, ujenzi wa mitambo na kujenga kituo cha kupoza umeme chenye uwezo wa kilovolti 400.

Kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme wa Rufiji kutapelekea kuwa na umeme mwingi na wa kutosha hivyo bei ya umeme itashuka na hivyo kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Aidha, utasaidia katika kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji miti kwani gharama za umeme zitashuka Wananchi watazimudu.

Inatarajiwa mradi huu utatumia asilimia 1.8 hadi 2 ya eneo lote la hifadhi.

Mradi huu pia utaongeza kasi ya kuunganisha umeme Wateja wa Vijijini na hivyo kufikia lengo la Serikali kufikia mwaka 2025 asilimia 85 ya wananchi wawe wameunganishiwa huduma ya umeme.