Uzinduzi RufijiSerikali imekabidhi rasmi eneo la mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (RHPP), kwa mkandarasi Kampuni ya Arab Contractors kwa pamoja na ile ya Elsewedy  Electric zote kutoka nchini Misri.

 Hatua hiyo sasa inaashiria kuanza kwa kazi ya ujenzi wa mradi huo wa umeme ambao utazalisha Megawati 2,115 ambazo zitaingizwa kwenye dridi ya Taifa na kuifanya Tanzania kuwa na umeme mwingi na wa uhakika.

 Akizungumza  wakati wa kukabidhi mradi huo kwa mkandarasi katika hafla iliyofanyika ndani ya Pori la Akiba la Selous, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema kuwa hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli kwa kusimamia uamuzi wa ujenzi wa mradi huo mkubwa.

 Alisema mradi huo ulibuniwa kwa muda mrefu tangu mwaka 1970 ambapo kazi ya uchambuzi ilifanyika lakini haukutekelezwa kwa sababu ya gharama zake kuwa kibwa.

 "Wakati ule (1970), mahitaji ya umeme yalikuwa megawati 100. Lakini leo mahitaji ya umeme ni makubwa sana. Na ilipangwa kwa wakati ule kutekelezwa kwa awamu ambapo ungeanza na megawati 400, awamu ya pili 800 na baadaye megawati 900. Hatua tuliyofikia leo ndiko serikali ya awamu ya tano inataka ya Tanzania ya viwanda

 "Huu ni mradi wa manufaa miji yote iliyozunguka mradi huu itakuwa kwa kasi sambamba na uzalishaji wa umeme," alisema

 Waziri huyo wa Nishati, alisema kuwa mkandarasi Arab Contractors, atafanyakazi ya kujenga bwawa la umeme ikiwamo kingo za kuta pamoja na kujenga vituo  ya kuzalisha umeme.

 "Ninapenda mtekeleze mradi huu kwa wakati na kwa ufanisi ili kuondoa mashaka kwa watu ambao wenye shaka. Leo mnakabidhiwa eneo la kazi ni matumaini yetu itaifanyakazi hii kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na umeme.

"Na kuanzia leo (jana) wakandarasi msiondoke site nyumba zipo, miundombinu ipo iwe jua, mvua jengeni mradi wakati wote na msiondoke hapa," alisema

Alisema pia kitajengwa kituo cha kupoza na kukuza umeme cha kV 400  na njia za kusafirisha umeme kwa msongo wa kV 400 kutoka eneo la mradi hadi Chalinze kwenda Dodoma na Dar es Salaam na utakamilika mwaka 2022.