Uzinduzi njia ya umeme Makambako hadi SongeaRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amezindua Mradi wa Ujenzi wa Njia Kuu ya Kusafirisha umeme wa kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea na vituo vya kupoza na kusambaza umeme.


Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kusimamia mradi huo ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Mikoa ya NJombe na Ruvuma Taifa kwa ujumla.


“Leo ni siku ya historia Mkoa wa Ruvuma, miaka ya nyuma suala la umeme Ruvuma lilikuwa tatizo”, alisema Mheshimiwa Rais.


Aliongeza mradi wa Makambako - Songea umeokoa shilingi Bilioni 9.8 kwa mwaka ambazo zilikuwa zikitumika kununulia mafuta ya kuendesha jenereta za kufua umeme.
Alisisitiza uhaba wa umeme una athari kwenye mazingira na kuongeza takribani hekari laki 4 za miti hukatwa kila mwaka hivyo uwepo wa umeme wa gharama nafuu utasaidia kuokoa mazingira.


“Ndugu zangu azma ya Serikali ni kuifanya nchi kuwa na umeme na kutosha, wa uhakika na gharama nafuu”, aliongeza Mheshimiwa Rais.
Akiuelezea mradi wa kufua umeme kwa njia ya maji wa Rufiji Hydropower utakao fua megawati zipatazo 2115, alisema mradi huo ni muhimu kwa Taifa kwani ukikamilika utatoa umeme zaidi ya tulionao sasa, hivyo ni lazima utekelezwe.


Aidha, eneo litakalojengwa mradi katika Mbuga ya Selous ni asilimia 2 lakini pia utasaidia kuokoa mazingira.


“Takribani watu laki 6 hupoteza maisha kutokana na matumizi ya mkaa, kuni na mafuta ya taa, lazima tuweke uwekezaji wa kutosha katika umeme”, alisema Mheshimiwa Rais.


Kwa upande wake Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, alisema mradi wa Makambako - Songea ilihusisha njia kubwa ya kusafirisha umeme wa kilovolti 220 umbali wa kilomita 250.


Aidha Wateja 22,700 wa awali watanufaika na mradi huu ambapo tayari vijiji 110 vimeunganishwa na Taasisi za Umma 114 na kazi ya usambazaji inaendelea.


Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi alisema, mradi umetekelzwa kwa kipindi cha miaka miwili (2) hadi kukamilika.


“Nia ya Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli ni kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2023, na hatuwezi kufika kwenye uchumi wa kati bila ya kuwa na umeme wa uhakika, sisi TANESCO tunawezeshwa kwa miradi mbalimbali mikubwa ikiwemo ule wa “Rufiji Hydro Power” utakaoongeza Megawati 2115 zitakazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.” Alisema Dkt. Kyaruzi.


Kukamilika kwa mradi wa kusafirisha umeme kutoka Makambako hadi Songea kutavinufaisha zaidi ya vijiji 122 hivyo kuondoa tishio la matumizi ya misitu kama nishati.


Mradi umegharimu shilingi bilioni 216 kati ya hizo shilingi bilioni 45 zimetolewa na walipa kodi wa Tanzania na zilizosalia zimetolewa kwa ufadhili wa Serikali ya Sweden.