Udhamini wa CRDB mradi wa RufijiMradi wa kufua umeme kwa maji wa Maporomoko ya Mto Rufiji (Rufiji Hydro Power Project) Mw 215 unaotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO umepata msukumo mpya baada ya benki za CRDB na UBA kutoa udhamini wa utekelezaji wa mradi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CRDB, Bw. Ally Leay akiwa na Mkurugenzi Mtedanji wa Benki hiyo, Bw. Abdulmajid M. Nsekela alimkabidhi hati za dhamana Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,  Dkt. Tito Mwinuka huku Mwenyekiti wa Bodi ya UBA, Balozi Tuvako N. Manongi akiongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Usman Isiaka naye alimkabidhi Hati kama  hizo Dkt. Mwinuka.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Aprili 15, 2019 kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt.  Hamisi Mwinyimvua, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi.Amina Shaaban, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dkt. Bernard Kibese, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles E. Kichere na Balozi wa Misri hapa nchini Mhe.Mohammed Gabel Abulwafa. Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo wanatoka nchini Misri.

Akizungumza kabla ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua alisema, dhamana hizo zilizokabidhiwa ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba utekeelzaaji wa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji wa mto Rufiji unaanza bila kuchelewa na kuhakikisha kwamba ratiba iliyokubaliwa baina ya serikali na mkandarasi inatekelezwa kwa mujibu wa mkataba.

“Mradi huu wa kufua umeme wa maji wa mto Rufiji wa megawati 2,115 ni muhimu sana kwa watanzania kwani umeme w amaji gharama zake ziko chini, hasa katika wakati huu ambao nchi yetu inaelekea kwenye uchumni wa viwanda.” Alisema Dkt. Mwinyimvua.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaaban alisema “Jambo hili ni muhimu sana la kuweka dhamana ya malipo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu kwani ni mradi wenye gharama kubwa kiasi cha shilingi za kitanzania trilioni 6.6 kwa hivyo ni mradi unaogharimu fedha nyingi katika historia ya nchi yetu katika miaka ya hivi karibuni.” Alisema Bi. Amina.

Kwa upande wake Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Benard Kibese alisema, kazi kubwa ya BoT katika utekelezaji wa mradi ni kuweka mazingira mazuri ili kuhakikisha ushiriki wa taasisi za fedha za hapa nchini unakuwa mkubwa.

“Leo niko hapa kushuhudia makabidhiano ya dhamana ya utekeleaji wa mradi wa umeme wa Rufiji, lakini pia siku ya leo ni muhimu sana kwa sababu inatuonyesha dhamira ya kweli ya serikali chini ya uongozi shupavu wa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, ndoto ya kufikia uchumi wa kati na wa viwanda unatimia, basi utekelezaji wake unahitaji fedha.” Alisema.

Naye Mkuurgenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka alibainisha kuwa TANESCO kama msimamzi wa mradi wa ujenzi wa umeme wa maji wa rufiji wa Megawati 2,115 hatua iliyofikiwa leo ni muhimu sana.

Aliishukuru serikali ya awamu ya tano chini wa uongozi wake Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwezesha hatua hiyo kufikiwa kwani mradi huu bila pesa kulipwa mkandarasi hawezi kufanya kazi yake hatua ya leo inawezesha pesa kulipwa kwa mkandarasi pale zitakapohitajika au pale ambapo mkandarasi anastahili kulipwa kwa hivyo kuanzia sasa utekelezaji wa mradi huu hautakuwa na kikwazo chochote katika ulipaji wa pesa, alisema Dkt. Mwinuka.