Wateja wakubwa MwanzaShirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewataka Wateja wote ambao hawajalipia bili zao za umeme kwenda kulipia au kufika katika Ofisi za TANESCO kujadiliana  namna ya kulipa madeni yao.

Akiongea na Waandishi wa Habari, Meneja Wateja wakubwa Mhandisi Fredrick Njavike, amesema TANESCO ipo kwenye mkakati wa kukusanya madeni yake na sasa kampeni hiyo imeanza katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Niwaombe Wateja wetu walipie bili
zao za umeme kwani Shirika haliwezi kujiendesha bila fedha “ alisisitiza Mhandisi Njavike.

Aidha, TANESCO inaendesha kampeni ya kubaini watu wanaojiunganishia umeme pasipo kufuata utaratibu.

Mhandisi Njavike alisema, TANESCO imekuwa ikipoteza mapato kutokana na baadhi ya watu kujiunganishia huduma ya umeme.

Aliongeza yeyote atakaebainika kutumia umeme kinyume na utaratibu sheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.

Aidha, katika kampeni hiyo, eneo la Igogo jijini Mwanza, Nyumba zinazomilikiwa na Kiwanda cha VOIL zilibainika kuwa na viashiria vya wizi wa umeme ambapo kwa mara ya mwisho umeme katika nyumba hiyo ulinunuliwa mwaka 2017.

Pia ilibainika jumla ya uniti 907 ambazo ni sawa na fedha zaidi ya laki tatu zikiwa zimetumika pasipo kuonekana kwenye bili zao.

Kwa upande wake  msimamizi wa nyumba hizo ambae ni fundi wa maswala ya umeme,  Bw.  Mzee Donge amekiri kuona hitilafu  katika mita na kusema kuwa hakua anajua na hivyo yupo tayari kulipa gharama hizo.