malipo wabunifu njombeShirika la umeme TANZANIA (TANESCO) limetekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alilotoa Juni 13 Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na wabunifu wa umeme kutoka Mkoani Njombe.

Mheshimiwa Rais aliwataka TANESCO kuwatembelea , kuwatambua , kuwapa ushauri wa kitalaamu pamoja na fedha mil 15 kila mmoja huku lengo kuu likiwa ni kuthamini na kutambua ubunifu na jitihada ambazo zimechukuliwa na watu hao kutimiza ndoto zao.

Akizungumza mbele ya umati wa wakazi wa Kijiji cha Lugenge wakati akikabidhi hundi ya fedha yenye thamani ya milioni pamoja na fedha taslimu milioni 5 kwa wabunifu wote wawili akiwemo John Fute maarufu Dr Pwagu na Laniel Ngailo mara baada ya kutembelea vituo hivyo vilivyobuniwa na watu hao Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Tito Mwinuka alisema Serikali itaendelea kuthamini na kutoa usaidizi wa kila hali ili kufikisha panapo stahili ndoto za wabunifu hao.

Aliongeza, timu hiyo ambayo imetumia siku mbili kutembelea na kukagua kitalaamu vituo hivyo vya kuzalisha umeme vilivyobuniwa kienyeji ambapo imejifunza mambo mengi ikiwemo uwepo wa watu wengi wabunifu ambao wanafanya mambo makubwa bila ya kujulikana na kuahidi kuwasaidia wabunifu hao kwa kila namna ili wawe na uwezo wa kuzalisha umeme mwingi zaidi utakaonufaisha na vijiji jirani.

“Watalaamu wa Shirika wamefanya utafiti na upimaji katika kituo cha Msete cha Bw. Pwagu pamoja cha Lugenge na kubaini vituo hivyo vikiboreshwa kisasa vinaweza kuzalisha kiwango kikubwa cha umeme utakaokuwa na manufaa kwa watu wengi", alisema Dkt. Mwinuka”

Kwa upande wao wabunifu hao ambao ni John Fute maarufu Pwagu na Laniel Ngailo walisema imekuwa kama ndoto kwa Mheshimiwa Rais wa Tanzania kutambua uvumbuzi na ubunifu wanaoufanya na kuamua kuwaunga mkono kwa kuwapa Wataalamu na fedha ili kuboresha huduma zao huku pia wakionesha hisia zao juu ya hatua ya TANESCO kuwakabidhi fedha taslimu mil 5 na hundi ya mil 10 kila mmoja kama ambavyo iliahidiwa mbele ya Rais Magufuli.

Aliongeza, wakati wameanza kujaribu kubuni miradi yao walikuwa wakidharauriwa na jamii zinazo wazunguka jambo ambalo limekuja kuwa nuru baada ya kutambuliwa na Rais hadi kuitwa Ikulu kuzungumza nao.

Katika timu iliyofika kwa wabunifu hao ilikuwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Emmauel Kalombelo ambaye pia alifurahishwa na ubunifu aliouona.

Aidha, alisema Serikali itaboresha mazingira yao ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Teknolojia.

Karakana ya Mzee John Fute maarufu Pwagu itaongezewa uwezo ili kiweze kuwa kituo kikuu cha ubunifu Mkoani Njombe na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini huku pia akiitaka Tume ya Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inawatambua wabunifu kutoka sekta mbalimbali waliopo nchini.

Mratibu wa masuala ya Habari na maarifa kutoka COSTECH Bw. Deusdedith Lenard alisema agizo hilo litatekelezwa haraka iwezekanavyo kwa kuanza mara moja uboreshaji wa kituo hicho cha ubunifu kilichopo nyumbani kwa Pwagu ili kiweze kutumiwa na watu wengi kubini vitu mbalimbali.

Ujio wa timu hiyo iliagizwa na Mheshimiwa Rais Juni 13 wabunifu walipokutana naye Ikulu kujadili masuala mbalimbali kuhusu Sekta Nishati.

Ubunifu wanaoufanya umewagusa wakazi wa Vijiji vya Lugenge na Msete mjini Njombe ambao wanasema wamefurahishwa na kitendo cha Mhe. Rais kutambua uwezo wa ndugu zao na kueleza kuwa uwezo wa umeme huo uliobuniwa kienyeji umekuwa msaada kwao.

Timu hiyo imewasili ikiwa na Watalaamu kutoka TANESCO, COSTECH, REA, Wizara ya Maji, Ewura na Mamlaka za Bonde la Mto Rufiji na Nyasa huku kila mmoja akitazama namna ya kuwasaidia wabunifu hao ambao wamekumbana na changamoto nyingi mpaka kufikia hapo.