uwekaji jiwe la msingi Katavi2Mradi wa Njia Kuu ya Kusafirisha Umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Ipole Tabora hadi Mpanda Katavi umbali wa kilometa 381 umezinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwekewa jiwe la msingi.


Uwekaji wa jiwe la msingi inaashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi huu wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 132 , ambao utagharimua shilingi Bilioni 135 fedha ambazo zitatolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Akizindua mradi huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, aliipongeza Wizara ya Nishati na TANESCO kwa kuutekeleza mradi wa Tabora - Katavi kwa kutumia Wataalamu wa ndani na uongeza hali hiyo itawajengea uwezo vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini.


Aliongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutafanya Serikali kuokoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 6.5 ambayo imekuwa ikitumika kwa mwaka kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme mkoani humo.


Aidha, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha Mkoa wa Katavi kupata umeme wa uhakika wa gridi utakaotosheleza mahitaji ikiwemo kuvutia wawekezaji watakao anzisha viwanda.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akitoa taaarifa ya mradi, alisema kuwa, Vijiji vitakavyopitiwa na mradi huo vitasambaziwa umeme huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi 27,000/=.


Aliongeza, mradi huo utakaotekelezwa na kampuni tanzu ya TANESCO ya ETDCO, pia unahusisha ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme ambacho kitafungwa transfoma mbili zenye uwezo wa megawati 50 kila moja ambapo mradi unatarajiwa kukamilika mwezi wa Tano mwaka 2020.


Mahitaji ya Mkoa wa Katavi ni takriban megawati 5, kupatikana kwa gridi ya Taifa Katavi itapata umeme wa kiasi cha megawati 100 hivyo kuwa na kiasi kikubwa cha umeme.
Hafla hiyo ulihudhuliwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu pamoja na Mawaziri kutoka Wizara mbalimbali, Wabunge, viongozi wa Mkoa wa Katavi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.