Waziri KAlemani na Waziri Zungu ziaraWaziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akiambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Mussa Azzan Zungu wamefanya ziara ya kikazi kwenye Vituo vya Kufua Umeme kwa maji vya Mtera na Kidatu.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua hali ya maji pamoja na athari za mazingira kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo kulazimu TANESCO kuruhusu maji kupita kwenye mkoando wake wa asili.

Akiongea katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Mazingira wameunda timu itakayoshirikisha Wataalamu mbalimbali itakayofanya kazi kwa siku kumi.

Aliongeza kuwa, Kamati hiyo ambayo ipo chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said itaangalia namna bora ya kuhifadhi maji kwenye bwawa hata baada ya kipindi cha mvua kupita.

Uhifadhi wa maji utaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na kuangalia namna bora ya kuwaelimisha wananchi wanaofanya shughuli za kijamii pembezoni mwa mabwawa ya kufua umeme pamoja na kwenye vyanzo vya maji.

"Wataalamu wameniambia maji haya yaliyopo kwenye bwawa la Mtera yapo kina mita 698.7 juu ya usawa wa bahari tukiyahifadhi vizuri yanaweza kuzalisha umeme kwa kipindi cha miaka mitatu ", alisema Dkt. Kalemani.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Mussa Azzan Zungu alisema kuundwa kwa Kamati hiyo lengo kubwa la Serikali ni kulinda mabwawa pamoja na uoto wa asili usipotee.

"Lazima maji ya kuzalisha umeme yapatikane kutoka kwenye vyanzo vya maji, Wananchi washiriki kutunza vyanzo vya maji", alisema Mhe. Zungu.

Aliongeza, nchi inategemea umeme kujiendesha hasa tunapoelekea kwenye uchumiwa Kati na wa viwanda na kusisitiza umeme wa majj ndio wa bei nafuu.