Hotuba ya budget 202021Bunge la Jamhuri ya Muungano waTanzania limepitisha jumla ya shilingi 2,196,836,774,00 kwa matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2020/21 ambayo ni ongezeko la asilimia 2.52 ya mwaka uliopita.

Akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema katika kipindi cha miaka mitano cha Serikali ya Awamu ya Tano, utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika Sekta ya Nishati imepata mafanikio makubwa.

Akiyataja mafaniko hayo ni kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme kutoka Mw 1,308 mwaka 2015 hadi kufikia Mw 1,601.84 Mwezi Aprili 2020, Kukamilika kwa Miradi ya Kuzalisha Umeme ya Kinyerezi I MW 150 na Kinyerezi II MW 240.

Mafanikio mengine ni Kuendelea na Ujenzi wa Mradi wa Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP) MW 2,115, Kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Rusumo MW 80 pamoja na kuunganisha Mikoa ya Lindi, Mtwara, Njombe na Ruvuma katika Gridi ya Taifa na hivyo kusitisha matumizi ya mitambo ya mafuta mazito ambayo ilikuwa inaigharimu
TANESCO wastani wa Shilingi bilioni 15.3 kwa mwaka.

Kwa upande wa umeme Vijijini Dkt. Kalemani alisema Serikali imeendelea na Utekelezaji wa Mpango Kabambe wa kusambaza umeme Vijijini ambapo hadi kufikia mwezi Aprili, 2020 jumla ya vijiji 9,112 vimeunganishiwa umeme ikilinganishwa na vijiji 2,018 vilivyokuwa vimeunganishwa umeme mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 351.54
Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 103 zimetengwa na Wizara kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye maeneo ya mijini ambayo yanasifa za kivijiji (pembezoni).

Dkt. Kalemani alibainisha baadhi ya majiji hayo ni Mwanza - Nyamagana, Dar es Salaam - Chanika na Mbeya.

Aliongeza hali ya upatikanaji umeme imeimarika ambapo hivi sasa hakuna mgao wa umeme na nchini inaziada ya umeme wa wastani wa megawati 325 kwa siku.

Akizungumzia suala la Wananchi kulipia nguzo Dkt. Kalemani alisema Serikali imegharamia kwa asilimia 100 na Wananchi hawapaswi kutozwa gharama za nguzo na kutoa rai kwa Wakuu wa Wilaya na Mkoa kuwachukulia hatua za kisheria mameneja watakao walipisha wananchi nguzo.

Alisema Serikali inampango wa kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la mfano "Kwa sasa Jiji la Dodoma lina megawati 42, tunajenga mtambo wa megawati 600 pale Zuzu na ukijumlisha na hizo 42, Jiji la Dodoma litakuwa na jumla ya Mw 642 ambazo hazijawahi kufikiwa kwa majiji ya Afrika", alisema Dkt. Kalemani.