Waziri Mkuu Tanzania inaongoza AfrikaWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Tanzania imeshika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kufanikiwa kusambaza umeme nchini kote kwa asilimia 80.

Mhe. Majaliwa aliyasema hayo wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenye mkutano wa viongozi wa dini kutoka kamati za amani za Mikoa mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar, uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

“Leo hii Tanzania ni ya kwanza barani Afrika kwa kusambaza umeme kote nchini hadi vijijini na kufikisha asilimia 80. Kuna nchi ngapi barani Afrika, lakini Tanzania imefanikiwa kuwa ya kwanza. Tumeweza kufikia vijiji 9,112 Tanzania na hadi Aprili 2020 na tumetumia shilingi trilioni 2.27,” amesema.

Akizungumza na viongozi waliohudhuria mkutano huo uliandaliwa ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake katika ustawi wa amani, uzalendo na kumtanguliza Mungu, Waziri Mkuu amesema ushirikiano mkubwa wanauonesha kwa Serikali, umewezesha kufanya mambo mengi ikiwemo kuimarisha huduma za upatikanaji wa nishati kwa ajili ya ustawi wa Watanzania.