Kilimanjaro waziri Agosti 2020Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Medard Kalemani ametoa siku 14 kwa wateja wote wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wenye malimbikizo ya bili za Umeme kuhakikisha wanalipa madeni yao ama kusitishiwa huduma baada ya muda huo kupita.

Waziri Kalemani ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa Miradi na kazi mbalimbali za Umeme Jijini Arusha.

“Natoa siku 14 kwa Wateja wote wa TANESCO Nchi Nzima wenye malimbikizo ya bili za umeme kulipa madeni yao. Baada ya muda huo kupita naagiza TANESCO kukata Umeme kwa wote watakaoshindwa kulipia madeni” Amesema Dkt. Kalemani

Waziri Kalemani aliongeza kuwa TANESCO ni Shirika la kibiashara ambalo linajiendesha kwa mapato yake bila kutegemea ruzuku ya Serikali hivyo kuchelewesha malipo ya bili za Umeme ni kuchelewesha juhudi za Shirika hilo kutekeleza ipasavyo majukumu yake ya kuwakwamua wananchi kiuchumi kupitia huduma bora na uhakika za Nishati ya umeme Nchini.

Dkt. Kalemani alimalizia kwa kusisitiza Wateja wote wakiwemo Wateja binafsi na Taasisi za Kiserekali kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati kwani muda wa kusitisha huduma kwa wasiolipa ukifika, TANESCO na Wizara hawatasikiliza wala kupikea simu za maelezo ya mdaiwa sugu yeyote yule isipokuwa kusitisha huduma ya Umeme mpaka deni litakapolipwa