Bodi ziara KigomaKutokana na Serikali kuwaamini wataalamu wa ndani (Watanzania) katika kutekeleza na kusimamia Miradi mikubwa na ya kimkakati, TANESCO imedhamiria kuinua uchumi wa Mikoa ya Magharibi kwa kuhakikisha inapata umeme wa kutosha, uhakika na gharama nafuu kwa kutumia Wataalamu kutoka TANESCO.

Wataalamu wa kitanzania wameonesha uwezo kwa kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo Mradi wa kimkakati wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere Mw 2115.

Safari ya kuhakikisha Mikoa ya Katavi na Kigoma ambayo ipo Kanda ya Magharibi inapata umeme wa uhakika ilianza Oktoba 11, 2019 baada ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa upelekaji umeme wa gridi ya Taifa Mikoa ya Kigoma na Katavi.

Kama ilivyo dira ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kuiona Tanzania ni nchi ya Viwanda, TANESCO inaiona ni dira ambayo itatukomboa Watanzania wote kwa uwepo wa umeme mwingi na wa kutosha.

Kutokana na ukweli kwamba nishati ya umeme ni uchumi na ni kichocheo cha maendeleo, Wananchi wanatakiwa kuchangamkia fursa ya kufika kwa umeme wa gridi ya Taifa katika Mikoa ya Katavi na Kigoma kwa kufungua biashara ambazo zitawaongezea vipato vyao.

Kwa kutambua umuhimu wa nishati ya umeme katika kukuza vipato vya Watanzania Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, imefanya ziara ya kikazi lengo likiwa kukagua miradi ya kusafirisha umeme Mikoa ya Katavi na Kigoma lakini pia na vituo vya kupoza na kusambaza umeme.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO Dkt. Alexander Kyaruzi alisema lengo la ziara ya Bodi ni kutaka kujiridhisha uhitaji mkubwa wa umeme kwa Mikoa ya Katavi na Kigoma hivyo Bodi kuweza kutoa uelekeo.

"Bodi imefika kuona mahitaji ya umeme kwenye Mikoa hii na kutafuta suluhu ya haraka”, alisema Dkt. Kyaruzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Katavi Mhe. Juma Homera akiwa kwenye kikao na Bodi ya Wakurugenzi TANESCO aliwaomba kuhakikisha umeme wa gridi unafika Mkoa wa Katavi kwa haraka kutokana na wawekezaji wengi kuonesha nia ya kufungua viwanda, pamoja na upatikanaji wa soko la chakula Kongo DRC.

Alisema, tayari wawekezaji wengi wameonesha nia akitolea mfano viwanda vya sukari, maji, kuchakata mpunga na mahindi lakini pia ujenzi wa Bandari kubwa ya Kalema.

Pia kiwanda cha kuchakata Pamba, uwekezaji wa krasha, ujenzi wa kiwanda cha nguo na ujenzi wa Reli kwenda ziwani Kalema”, alisema Mhe Homera.

Miji ya Katavi na Kigoma ni miongoni mwa miji inayopata maendeleo kwa kasi hivyo uhitaji wa umeme wa gridi kwenye Mikoa hiyo ni mkubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ameipongeza Bodi na Menejimenti ya TANESCO, aliesma kupatikana kwa umeme wa uhakika Mkoa wa Kigoma kutawawezesha Wananchi kukuza vipato vyao.

Mhandisi Sana Idindili ambaye ni Meneja Mwandamizi Kanda ya Magharibi akitoa taarifa kwa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO alisema Mkoa wa Katavi unapata huduma ya umeme kupitia vyanzo viwili vya jenereta zinazo tumia mafuta kufua umeme katika Wilaya za Mpanda na Mlele na umeme wa gridi ya Taifa kutokea nchini Zambia kupitia Mkoa Rukwa.

Gharama za uzalishaji umeme kwa Mkoa wa Katavi kwa unit moja ni wastani wa shilingi 750.

Aliongeza kuwa, kwa upande wa Mkoa wa Kigoma unapata huduma ya umeme kupitia vyanzo vitatu ambavyo ni Kigoma mjini, Kasulu na Kibondo na vituo vyote vinazalisha umeme kupitia mafuta. Gharama ya kuzalisha umeme kwa wastani unit moja ni shilingi 649.4.

Umeme utakao patikana kupitia gridi ya Taifa ni wa uhakika na unapatikana kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo maji na gesi.

Kampuni Tanzu ya TANESCO ya ETDCO ndio itakayohusika na ujenzi wa Njia Kuu ya Kusafirisha kutoka Tabora hadi Katavi na Kutoka Tabora hadi Kigoma.

Wataalamu wa TANESCO watahusika na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Ipole, Ingonga, Mpanda, Urambo na Nguruka.