Mkutano na Waandishi wa Habari Agosti 28Na Grace Kisyombe, Dar es salam.

Bodi ya Wakurugenzi  ya TANESCO imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kupambana na wizi  pamoja na hujuma katika miundombinu ya umeme.

Akizungunza katika mkutano na  Waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Dkt. Alexander L. Kyaruzi  amesema Bodi ya Wakurugenzi kupitia kamati zake imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kupambana na hujuma katika miundombinu ya umeme,


“Baadhi ya taasisi zinazoshiriki katika kampeni maalum ya kukamata wahujumu miundombinu ya umeme ni, Jeshi la Polisi, Takukuru, Ofisi ya Mwendesha mashtaka wa Serikali (DPP), Idara ya Usalama wa Taifa pamoja na wataalam wengine kutoka TANESCO na Wizara ya Nishati” Amesema Dkt. Kyaruzi

Dkt Kyaruzi aliongeza kusema kuwa, kikosi kazi hicho kitakuwa na jukumu la kukamata na kuwafikisha mahakamani wale wote wanao jihusisha na wizi pamoja na uharibifu wa miundombinu ya umeme.

Kikosi kazi hicho kimeanza kufanya kazi katika Mkoa wa Dar e salam, ambapo tayari watuhumiwa wanne wamekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi.

Katika hatua nyingine Dkt. Kyaruzi amewaomba wananchi na wasamaria wema kushiriki katika kampeni hii kwa kutoa taarifa za siri ambazo zitafanikisha kuwakamata wananchi wanao hujumu miundmbinu ya umeme.

Dkt Kyaruzi amesema kuwa kutakuwa na zawadi ambazo zitakuwa zikitolewa kwa wale wote watakao fanikisha kukamatwa kwa watu wanao hujumu  miundombinu ya umeme.

Zawadi hizi ni za fedha tasilimu na kiwango cha zawadi hizi kitategemea ukubwa wa mali iliyo kamatwa au kuokolewa kutoka katika hujuma hizo.

Aidha, Dkt. Kyaruzi amewakumbusha wananchi wote wenye madeni ya umeme kulipa madeni hayo haraka kwani muda wa siku 14 ulio tolewa na Mhe Waziri wa Nishati unakaribia kwisha, hivyo basi kuanzia  Septemba 1, 2020 TANESCO itakata umeme kwa kila anaye daiwa, zoezi hili litahusu taasisi, wafanyabiashara na watu binafsi wanao daiwa.