Ziara ya Menejimenti TANESCO JNHPP

Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imefanya ziara ya kukagua hatua iliyofikiwa katika utekelezaji mradi wa kufua umeme wa Megawati 2115 kwa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) na kuonyesha kuridhishwa na kuikubali kasi ya utekelezaji wa mradi huo kulingana na mpango kazi uliopo.

Akiongea katika ziara hiyo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji na Huduma kwa Wateja, Mhandisi Raymond Seya, amesema kuwa ziara hiyo ina malengo mawili ambayo ni, kukagua hatua za utekelezaji wa mradi na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Bodi ya Wakurugenzi TANESCO.

Mhandisi Seya ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka, aliongeza kuwa, Menejimenti imeridhishwa na hatua za utekelezaji wa mradi tangu kuanza kwake ambapo ni zaidi ya mwaka na miezi mitano sasa.

“Mradi upo katika hatua nzuri, tumekagua maeneo mbalimbali mradi unapotekelezwa na tumejiridhisha, kazi zinaendelea na mradi utakamilika kama ilivyopangwa, Juni 2022” amesema Mhandisi Seya.

Mhandisi Seya aliongeza kuwa, Menejimenti ya TANESCO inaishukuru Serikali kwa kumlipa Mkandarasi kwa wakati bila kumcheleweshea malipo, hali ambayo inachangia kasi ya utekelezaji wa mradi kwa Wakandarasi kuongezeka.

Kwa upande wa Mkuu wa Kazi za Ujenzi TECU, Mhandisi Lutengano Mwandambo alisema kazi za ujenzi wa mradi zinaendelea vizuri na kuongeza kuwa, ujenzi wa handaki la kuchepusha maji umefikia asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 25 mwaka huu.

“Handaki hili la kuchepusha maji ni muhimu katika utekelezaji wa mradi huu, kwani ndio litawezesha ujenzi wa tuta la kuzuia maji kujengwa, tunatarajia hadi kufikia Oktoba 25 mwezi huu kazi ya kumimina zege kwenye handaki itakuwa imekamilika” amesema Mhandisi Mwandambo.

Aidha, Mkandarasi amechukua hatua muhimu badala ya kusubiri maji kuchepushwa kwenye handaki, tayari ameanza ujenzi wa tuta sehemu ya pembeni mwa mto tangu Oktoba 13, 2020.

Ziara ya Menejimenti inafuatia ziara ya Bodi ya Wakurugenzi TANESCO kwenye mradi wa Julius Nyerere Oktoba 04, 2020, ambapo Bodi ilitoa maelekezo ya kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.