KUSAINI MKATABA KATI YA TANESCO NA WAWEKEZAJI WADOGOShirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeingia mkataba wa kununua umeme kutoka kwa wazalishaji wadogo wa kampuni sita binafsi, utakaoingia moja kwa moja kwenye kwenye gridi ya Taifa na kutumika katika maeneo mbalimbali Nchini.

Akizungumza katika hafla fupi ya kusaini mikataba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Meneja Mwandamizi Uwekezaji, Mhandisi Costa Rubagumya alisema wawekezaji hao wamekidhi vigezo kwa mujibu wa kanuni zilizoidhinishwa na EWURA.

"Kwa mujibu wa kanuni zinazosimamia uendelezaji wa miradi midogo ya kuzalisha umeme, inaitaka TANESCO kuingia mikataba na wazalishaji umeme wadogo kwenye maeneo ambayo gridi ya Taifa bado haijafika", alisema Mhandisi Rubagumya.

Aliainisha vigezo vingine ni maeneo ambayo yanatatizo la umeme mdogo ili kuimarisha ubora wa umeme na kigezo kingine ni maeneo ya usambazaji umeme ambapo  njia za umeme za TANESCO ni ndefu hivyo kusababisha upotevu wa umeme.

Mhandisi Costa alizitaja kampuni hizo kuwa ni, Kahama Solar Power Project MW 10.0, Kigoma Solar Power MW 5.0, Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd MW 0.36.

Makampuni mengine ni, Madope Hydropower MW 1.7, Luponde Hydropower MW 0.9 na Maguta Hydropower MW 1.2.

Wakizungumza Kwa niaba ya Wazalishaji wadogo wa umeme, Padre Luciano Mpoma na Nicholas Richardson wameishukuru Serikali kupitia TANESCO kwa kukubali kufanya nao biashara ya umeme.

Waliongeza kuwa safari ilikuwa ni ndefu lakini hatimaye wamekuwa na furaha kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha nishati ya umeme inamgusa kila mwananchi.

Makampuni hayo yanatakiwa kuanza kuiuzia TANESCO umeme ndani ya miezi 18 kuanzia leo Disemba 08, 2020.