Waziri ziara JNHPP Desemba 2020Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani Desemba 14, 2020 akiwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua umeme wa Megawati 2115 kwa njia ya maji wa Julius Nyerere, amesema inatarajiwa kwa mwaka 2023 mahitaji ya umeme Nchini yakaongezeka kwa zaidi ya mara mbili mpaka kufikia megawati 2,770.

"Leo hii mahitaji kwa siku ni megawati 1,177.20. Kukamilika kwa mradi huu wa Julius Nyerere kutaongeza megawati 3,973 ambazo zitatumika katika shuguli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii hivyo tunahitaji umeme wa kutosha, utakaobaki tutawauzia majirani zetu" amesema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani aliongeza kuwa, mradi wa Julius Nyerere utapeleka umeme kwenye gridi ya Taifa pamoja na kwenye miundombinu yenye uhitaji wa umeme kwa gharama nafuu.

Pia umeme huo utapelekwa kwenye vijiji 12,0268 Nchi nzima pamoja na kwenye Vitongoji vyake ambavyo ni vinafikia 64,0889.

Aidha, Dkt kalemani ameeleza kuwa, kutokana na umeme wa maji kuzalishwa kwa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine, inatarajiwa kukamilika kwa mradi kutasaidia kushusha bei ya umeme kwa watumiaji.

Katika hatua nyingine Dkt. Kalemani ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi TANESCO pamoja na Katibu Mkuu Wizara Nishati, kuunda timu ya kufuatilia utengenezaji wa mashine zitakazofungwa kwa ajili ya kufua umeme ili kuepuka ucheleweshaji mradi.

Akitoa tathmini ya jumla ya utekelezaji wa mradi, Waziri Kalemani amesema kiujumla mradi unaendelea vizuri ambapo eneo la uchepushaji maji limekamilika kwa asilimia 100, wakati eneo la ujenzi ambapo bwawa linahitajika kujengwa umbali wa mita 1,045 pamoja na kimo cha mita 131 unaendelea vizuri.

Kwa upande wake Naibu Waziri Nishati, Mhe. Stephen Byabato, ameelezea kufarijika na kasi ya ujenzi wa mradi huo na kuahidi kusimamia maagizo ya Waziri ili kuona yote yaliyoagizwa yanatekelezwa kwa wakati, ubunifu mkubw na kwa usahihi.