Waziri Makamba TaboraWaziri wa Nishati Mhe. January Makamba leo Mei 19, 2022 ameshiriki ziara ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Samia Suluhu Hassan Mkoani Tabora ambapo amewahakikishia wananchi kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa umeme nchini kupitia uwekezaji wa miradi ya umeme inayoendelea.
 
Akitoa salamu za Wizara ya Nishati Waziri Makamba amesema upatikanaji wa nishati ya umeme unategemea mambo matatu muhimu ambayo ni uzalishaji, usafirishaji na usambazaji.
 
"Uhakika wa upatikanaji wa umeme unategemea uimara wa miundombinu ya usafirishaji na uzalishaji wa umeme unaotosheleza" amesema Mhe. Makamba.
 
Ameongeza kuwa changamoto kubwa ya upatikanaji wa umeme nchini inatokana na uwepo wa miundombinu chakavu na isiyotosheleza mahitaji.
 
Amesema kwa muda mrefu Serikali haikufanya uwekezaji kwenye maeneo ya uzalishaji na miundombinu unaoendana na wakati pamoja na mahitaji ya kutosheleza.
 
"Mfumo wetu wa gridi umeelemewa kutokana na uchakavu ambao unasababisha maeneo mengi ya nchi yetu umeme kufika ukiwa umefifia na mwingi unakuwa unapotea njiani" amesisitiza Mhe. Makamba.
 
Akielezea changamoto za umeme ambazo zinazikabili Wilaya za Urambo na Kaliua Mkoani Tabora, Waziri Makamba amesema tatizo la kukatika kwa umeme katika Wilaya hizo zinatokana na njia ya umeme kutembea umbali mrefu takribani umbali wa kilometa 1,200.
 
"Tangu nchi yetu ipate uhuru mahitaji ya umeme yamekuwa yakiongezeka kila wakati, katika kipindi cha miezi sita iliyopita tumevunja rekodi ya mahitaji ya umeme mara nne, tumefikia mahitaji ya megawati 1,336 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa.
 
Amesisitiza hii inamaanisha shughuli za uchumi zinaongezeka kwa watu kufungua biashara na uwekezaji katika viwanda.
 
Kuhusu kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme Waziri Makamba amesema Serikali imeweka mpango wa kurekebisha gridi wenye thamani ya takribani dola bilioni 1.9.
 

Mpaka sasa Serikali tayari imeshatenga kiasi cha shilingi bilioni mia 500  kwa mwaka ujao wa fedha 2022/2023 kutekeleza miradi mbalimbali itakayosaidia kuimarisha hali ya upatikanaji umeme kwenye gridi ya Taifa.