Waziri Mkuu Maonesho Nishati 2022Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameeleza kufurahishwa na maonesho ya siku tatu ya Wizira ya Nishati na taasisi zake yaliyofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma kuanzia Mei 23 hadi 25, 2022.
 
“Nimefurahishwa kuona jambo hili ambalo Waziri wa nishati January Makamba alilieleza Bungeni kuhusu kuweka utaratibu kwa waheshimiwa wabunge kujua shughuli za Wizara na taasisi zake katika maeneo yao ,” amesema Waziri Mkuu.
 
Waziri Mkuu ameongeza kuwa, ubunifu wa kuweka  maonesho hayo umesaidia wabunge kufahamu mambo yanayoendelea ndani ya Wizara ya Nishati hususani katika taasisi zilizopo chini ya Wizara ya nishati na maeneo mengine.
 
Akieleza juu ya umuhimu wa maonesho hayo kwa wabunge, Waziri Mkuu amesema kuwa wabunge watakuwa na nafasi ya kuchangia kwenye mjadala utakaohusu Wizara ya Nishati bungeni wakiwa na uelewa mpana wa mambo yanayofanywa na Wizara hiyo.
 
“Wote tunafahamu wabunge wanataka kujua umeme unapatikana lini katika maeneo yao, hii inahusisha mlolongo mzima wa upatikanaji umeme kuanzia uzalishaji, usafirishaji na usambazaji mpaka kumfikia mteja,” amesema Waziri Mkuu.
 
Aidha,Waziri Mkuu amesema kuwa amewaona mameneja wa kanda na mikoa ya kitanesco wakieleza hatua iliyofikiwa ya uunganishaji umeme kwa wateja wapya katika maeneo yao.
 
Amewasihi wataalamu waliokuwa kwenye maonesho hayo watakaporudi kwenye maeneo yao ya kazi wahakikishe wanafanyia kazi changamoto walizopewa na wabunge na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
 
“Kama tutakuwa na maelezo mazuri lakini bila ya kuwa na matokeo bado itakuwa haina tija zaidi ni vyema kuweka mpango kazi kufikia hatua ambayo Serikali inahitaji,” amesema Waziri Mkuu.
 

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati January Makamba akimkaribisha Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa mwitiko wa wabunge kwa siku zote za maonesho umekuwa mzuri, huku wabunge wakipata fursa ya kupatiwa majawabu ya changamoto mbalimbali walizonazo majimboni kwao.