loading...

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Tarehe 21 Machi, 2024 wameingia kwenye ubia ili kuanza utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa kusambaza umeme kwenye nyumba 5,000 katika kijji cha Msomera, Saunyi na Kitwai B, wilayani Handeni, mkoani Tanga ambapo Mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 48.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema, Mradi huo utakuwa endelevu na kuongeza kuwa licha kuwafikishia Wananchi huduma ya umeme katika vijiji hivyo lakini pia utawaunganisha Wananchi na huduma ya umeme (Wiring) moja kwa moja kwenye nyumba zao bila ya wao kulipia huduma hiyo.

“Nyumba 5,000 zitasambaziwa umeme pamoja na kufanyiwa “wiring”. Lengo la Serikali ni kuhakikisha Wananchi katika vijiji hivyo, mnapata umeme lakini pia mnaishi vizuri na kufanya shughuli zenu za kiuchumi”. Amesema Naibu Waziri Kapinga.

Naibu Waziri Kapinga amewaambia wakandarasi wanaotekeleza Mradi huo kuongeza kasi katika kazi hyo pamoja na kutanguliza weledi katika majukumu yao.

“Tekelezeni Mradi huu kwa wakati ili Wananchi wapate umeme kwa wakati, tunawategemea mfanye kazi kwa weledi, (Sisi) Viongozi wa Wizara ya Nishati, tupo pamoja nanyi ili kuhakikisha Miradi hii yote, inakamilika kwa wakati”. Amekaririwa Naibu Waziri, Kapinga.

Mradi huo mkubwa utatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia mkandarasi, kampuni ya China Railways Construction and Electrification Bureau Group Company Ltd (CRCEBG) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kampuni yake tanzu ya ETDCO.