loading...

TANESCO YAMKABIDHI MKANDARASI UJENZI WA NJIA YA UMEME CHALINZE -DODOMA

Na. Shamu Lameck
Pwani
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya makabidhiano kwa Kampuni ya TBEA ya China  Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 345 kutoka kituo cha Kupokea na kupoza umeme cha Chalinze kuelekea Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo April 17, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha. Gissima Nyamo-Hanga amesema kwa sasa kituo cha Chalinze kinaweza kubeba megawati 850, hivyo mradi ukikamilika umeme wote kutoka Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere utaweza kusafirishwa kupitia njia hiyo ya chalinze - Dodoma na kufikishwa katika maeneo mengine ya nchini.

"Mradi huu ni mkubwa una kilometa 345 na gharama yake ni bilioni 510 za kitanzania, sisi kama watumishi tunaowajibu mkubwa wa kuhakikisha tunasimamia rasilimali hii ya Serikali amabyo inawekwa hapa kwa ajili ya watanzania," amesema Mha.Gissima

Ameeleza kuwa umeme huo utasafirishwa kupitia njia hiyo kwenda kwenye Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu kilichopo jijini Dodoma na kuwa baada ya umeme kufikishwa hapo itakuwa rahisi kufika maeneo mengine ya nchini.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Dkt. Rhimo  Nyansaho amesisitiza mradi huo kukamilika kwa wakati huku akiitaka menejimenti ya TANESCO kusimamia kwa ukaribu zaidi ili kubaini changamoto mapema kama zikitokea.

"Kutokana na umuhimu wa njia hii ya kutoka chalinze kwenda Dodoma, tumsisitize Mkandarasi kwamba kazi hii inachukua miezi isiyopungua 22, fedha zipo kila kitu kipo tuhakikishe anaweza kumaliza hii kazi ndani ya miezi 22,” amesema Dkt. Rhimo Nyansaho

Ameongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na njia za kusafirisha umeme zenye ubora ili kuwezesha umeme unaozailishwa kwenye vyanzo mbalimbali unakuwa na tija.

"Tulichokikwepa ni kuwa na maneno mengi mwisho wa siku watanzania wanataka umeme," amesisitiza Dkt. Nyansaho.