loading...

"MNAFANYA KAZI KUBWA, MUENDELEE KUJITANGAZA ZAIDI ILI WANANCHI WAFAHAMU SHUGHULI MNAZOZIFANYA "– Mha. Luoga"

Na Charles Kombe, Dar es Salaam

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya nishati, Mha. Innocent Luhoga ameipongeza TANESCO pamoja na kampuni zake tanzu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme unakuwa wa uhakika na kuwataka kuongeza nguvu kwenye kutoa taarifa kwa umma juu ya kazi wanazozifanya.

Mha. Luoga ameyasema hayo Julai 5, 2024 alipotembelea banda la TANESCO katika maonesho ya 48 ya kimataifa ya Sabasaba ambapo alipata fursa ya kupata maelezo mbalimbali juu ya uzalishaji wa umeme hapa nchini.

“TANESCO mnafanya kazi kubwa, REA wanafanya kazi kubwa, Joto Ardhi wanafanya kazi kubwa, ITDCO wanafanya kazi kubwa lakini wananchi wanatakiwa kuzifahamu kazi mnazozifanya hivyo ongezeni kujitangaza  kazi mnazozifanya kwa umma. Ni wachache wanaopata nafasi ya kuja kwenye maonesho haya hivyo wale wasiokuja hawajua miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa na Serikali” amesema Mha. Luoga

Mha. Luoga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha miradi mikubwa ya kuzalisha umeme inatekelezwa.

“Nimeona miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme inayotekelezwa na TANESCO ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme pamoja na miradi ya baadae inayotarajiwa kutekelezwa lakini pia nimeona namna ambavyo Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo” amesema Mha. Luoga

Akiongea kuhusu upatikanaji wa umeme nchini Mha. Luoga amesema dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya nishati imezidi kuonekana ikiwa ni pamoja na kuingizwa kwenye gridi ya taifa umeme kutoka katika mradi wa bwa wa la kufua umeme la Julius Nyerere.

“Tumeona mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere tayari mashine mbili zimeshaanza kuzalisha umeme wa megawati 470 na hivyo kuondoa tatizo la umeme nchini. Tumekua na mgao wa umeme kwa kipindi fulani lakini kutokana na utekelezaji wa mradi huu tatizo hilo halipo tena” ameongeza Mha. Luoga.

TANESCO inaendelea kushiriki katika maonesho ya Sabasaba na imeendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake ili kuweza kupata maelezo muhimu juu ya huduma za umeme pamoja na kufahamu miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.