
Dar es Salaam
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuanza kwa kampeni maalumu ya uhamasishaji ulipaji wa madeni na ulinzi wa miundombinu inayokwenda kwa jina la “ Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie “ yenye lengo la kuhamasisha uwajibikaji wa pamoja katika kulipa bili na kulinda miundombinu kwa huduma endelevu ya umeme.
Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi leo , tarehe 19 Juni 2025 na inajikita katika maeneo yote nchini, ambapo kaulimbiu ya kampeni hiyo ni “Huduma endelevu huanza na wewe” ikilenga kuhimiza uwajibikaji wa pamoja kati ya Shirika na wateja wake.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja TANESCO Bi. Irene Gowelle amesema, lengo la kampeni ni kuhimiza wateja wanaodaiwa kulipa madeni yao kwa hiari kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
“Tumefungua milango ya msamaha wa riba, tunawahimiza wateja wetu wenye madeni ya muda mrefu kutumia fursa hii kuweka makubaliano ya ulipaji kwani kufanya hivyo kutawaepusha na hatua za kisheria pamoja na usumbufu wa kusitishiwa huduma,“ amesisitiza Bi. Irene.
Sambamba na hilo, ameeleza kuwa TANESCO itafanya pia ukaguzi wa mita za LUKU kwa wateja wa mfumo wa malipo ya kabla, ili kubaini mita zilizochezewa au zenye hitilafu, nakuchukua hatua stahiki kwani wizi wa umeme na matumizi ya mita zilizochezewa ni chanzo cha hasara kwa Shirika unaoathiri ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Katika hatua nyingine, Bi. Gowelle amesema kampeni hiyo inajumuisha pia uhamasishaji wa ulinzi wa miundombinu ya umeme kupitia elimu kwa jamii juu ya wajibu wao katika kulinda rasilimali za umma.
“Ni vema mfahamu kuwa, ulinzi wa miundombinu ya umeme ni jukumu letu sote ni wajibu wa kila mwananchi. Kulinda miundombinu ni kulinda upatikanaji wa huduma endelevu ya umeme kwa wote ili kuchochea uchumi wa nchi na kuwezesha shughuli za kila siku za wateja,” ameeleza Bi. Gowelle.
Akifafanua ameeleza kuwa matukio ya wizi wa miundombinu ya umeme yamelisababishia Shirika hasara ya kiasi cha shilingi milioni 770 katika kipindi cha Juni hadi Disemba, 2024 akitaja wizi wa transfoma kukithiri zaidi ambapo idadi ya kesi 63 zimeripotiwa huku mashauri nane (8) yakiwa mahakamani.
Aidha amewahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uharibifu au wizi wa miundombinu ya umeme ili kuzuia athari na hasara kwa Shirika na jamii kwa ujumla.