loading...

BITEKO: MGAO WA UMEME KUISHA HIVI KARIBUNI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Biteko amesema kuwa Mgao wa Umeme upo ukingoni kuisha kwa kuwa Serikali imeshafanya jitihada kubwa ya kukabiliana na changamoto ya Umeme ikiwa ni pamoja na kuwekeza fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya Umeme.

Mhe Biteko ameyasema hayo Februari 23 ,2024 alipoambatana na Waziri wa maji Mhe Juma Aweso kwenye ziara ya kukagua Bwawa la kuzalisha Umeme la Kidatu na kuwataka watanzania kuvumilia kidogo changamoto ya umeme ambayo inakwenda kuisha.

“Serikali ya Awamu ya sita ya Mhe Dkt Samiah Suluhu Hassan imeshatoa fedha nyingi kwajili ya kukabiliana na changamoto ya Umeme nchini, niwaombe wananchi kuvumilia  kidogo, suala la mgao wa Umeme linakwenda kwisha!"Alisema Mhe.Biteko

Aidha  Mhe. Biteko ameridhishwa na kiwango cha maji kilichopo katika Bwawa la Kidatu,maji ambayo pia yatatumika kufua umeme katika Bwawa la Julius Nyerere, kupitia mikondo ya maji ya mto ruaha mpaka kufika mto Rufiji.

Kadhalika Mhe .Biteko ametoa onyo kali kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kuchepusha mito ya maji inayokwenda kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme kwa shughuli zao binafsi  pamoja na kufanya shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji, vitendo vinavyoharibu vyanzo vya maji.

“Hatutawafumbia macho watu wanaoharibu vyanzo vya maji, kwani unasababisha ukame katika mabwawa haya na lawama zinaishia kwa TANESCO na Serikali, hivyo tutunze vyanzo vyetu vya maji”.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Awessu, ameahidi kushirikiana na wizara ya Nishati katika kutokomeza ukame,katika mabwawa ya kuzalisha Umeme, lakini pia katika kuhakikisha maji yanapatikana kwa wananchi wote kwani Umeme na maji ni sekta zinazotegemeana.