
MD TWANGE AWAHAKIKISHIA WANANCHI WA MIKOA YA KUSINI UMEME WA UHAKIKA
Ni baada ya kusafirishwa kwa Mtambo wa kuzalisha umeme kwa gesi asilia wa megawati 20
Atoa rai kwa watendaji wa TANESCO kupambana na wizi wa umeme na uharibifu wa miundombinu
Na Josephine Maxime, Lindi
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange amewaondoa hofu wananchi wa Mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara kuwa Mikoa hiyo itaendelea kuimarika kwa kupata umeme wa uhakika baada ya kuongeza Mtambo wa kuzalisha gesi asilia wa Megawati 20 unaotarajia kuwasili Mkoani Mtwara hivi karibuni.
Hayo aliyasema Septemba 15, 2025 alipofanya ziara katika Mikoa ya Kusini ambapo akiwa katika Mkoa wa TANESCO wa Pwani Kusini eneo la Mkuranga Mkurugenzi Mtendaji alieleza kuwa licha ya mchango mkubwa unaofanywa na wafanyakazi amewataka kuongeza kasi ya kupambana na matukio ya wizi wa umeme ambayo yamekuwa yakiripotiwa.
"Endeleeni kupambana na wezi wa umeme ninyi mnahangaika na kazi ya kuwafikishia umeme lakini wapo watu ambao wanafanya vitendo vya wizi kwa lengo la kulipa kiasi kidogo tofauti na matumizi ili TANESCO isipate mapato yake kihalali,"alieleza Bw. Twange.
Katika hatua nyingine alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainabu Telack na kumhakikisha kuwa licha ya Mtambo wa kuzalisha umeme wa Megawati 20 utakaopelekwa kuongeza uzalishaji wa umeme TANESCO inafanya jitihada za makusudi za kuendelea kuboresha njia za kusafirisha umeme katika Mkoa huo.
‘’Tunafahamu changamoto zilizopo tutahakikisha kwa kutumia miundombinu iliyopo tutaimarisha hali ya upatikanaji umeme kwa Mkoa wa Lindi, tunao mpango mkakati ambao unaonesha jitihada zinazoendelea kufanyanyika na hivi karibuni utaanza kuona matokeo,’’ alifafanua Bw. Twange.
Mkurugenzi Mtendaji ametumia sehemu ya ziara yake kutoa majiko yanayotumia umeme kidogo kwa baadhi ya viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji kwa lengo la kuendelea kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya umeme kupikia ambayo ni nafuu na ni rafiki wa mazingira.