
Aifikia mikoa ya Ruvuma na Mtwara
Akagua miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuifikisha elimu ya nishati safi ya kupikia kwa umeme
Na Josephine Maxime
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange ameendelea na Ziara yake katika mikoa ya kusini mwa Tanzania ambapo amekagua miradi mbalimbali ya umeme, kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa umeme pamoja na kuzungumza na wafanyakazi ili kuboresha ufanisi wa kuwahudumia watanzania.
Akiwa mkoani mkoani Ruvuma Bw. Twange alikagua maendeleo ya Kituo cha kupoza umeme cha Songea – Tunduru ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 50.6 ya utekelezaji wake ambao utakapokamilika utachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme mikoa yote ya kusini.
Aidha, alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Brigedia Jenerali Ahmed Abas Ahmed ambapo miongoni mwa mengi waliyozungumza alielezea juu ya namna TANESCO imejipanga kuimarisha umeme katika Mkoa wake, Mkurugenzi Mtendaji alimkabidhi jiko la umeme linalotumia umeme kidogo ikiwa ni jitihada za kuendeleza kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Hatahivyo katika Mkoa wa Mtwara alizitambua changamoto mbalimbali za umeme mkoani humo pamoja na kueleza namna zinakwenda kutatuliwa kutokana na miradi ya umeme inayoendelea.
Alifanya pia mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Partick Sawala ambapo alimhakikishia kuwa TANESCO imejipanga kuimarisha hali ya umeme katika Mkoa wake ikizingatiwa imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kutatua changamoto za umeme Mkoani humo.
Huu ni mwendelezo wa Ziara za Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO mikoa ya kusini ambazo zimeleta matokeo makubwa kwa wafanyakazi wa TANESCO katika utendaji kazi ambapo mazingira yao ya kazi yameimarishwa kwa kiasi kikubwa huku changamoto zao zikitatuliwa lakini pia utambuzi wa changamoto mbalimbali zinazofanya ukosefu wa umeme mikoani humo na mwarobaini wa tatizo hilo.