
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu avutiwa na teknolojia ya majiko bora ya umeme
Katika maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2025 yanayoendelea katika Viwanja vya Uhindini, mkoani Mbeya, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wananchi na vijana wanaotembelea banda lake.
TANESCO kupitia wataalamu wake limekuwa likitoa mafunzo kwa vitendo kuhusu namna ya kutumia majiko bora ya kisasa yanayotumia umeme kidogo, salama kwa mtumiaji, na rafiki kwa mazingira.
Akitembelea banda la TANESCO Oktoba 9, 2025, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Mary Mongela Maganga, alipongeza juhudi hizo, akisisitiza kuwa elimu ya matumizi ya nishati safi ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya taifa, hasa katika kulinda afya za wananchi na mazingira.
"Nimevutiwa na teknolojia ya majiko haya ya kisasa yanayotumia umeme kwa ufanisi mkubwa". Amesema Bi. Mary.
Ameongeza vijana wanapaswa kutumia fursa ya maonesho haya kujifunza teknolojia hizo ili kuzitumia katika maisha yao ya kila siku na katika ujasiriamali.
TANESCO imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia inawafikia wananchi wengi zaidi nchini kote, sambamba na juhudi za serikali za kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034)