Na Constantine James
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, Januari 28, 2026 alifungua rasmi kikao kazi cha Waandishi Waendesha Ofisi wa TANESCO kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Midland, Jijini Dodoma.
Akifungua kikao hicho, Bw. Twange amewataka Waandishi Waendesha Ofisi kuzingatia kwa umakini sheria na taratibu za kiutumishi, ikiwemo kulinda siri na nyaraka zote za Shirika, jambo litakalosaidia kuboresha utendaji wa kazi ndani ya TANESCO.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, akibainisha kuwa Waandishi Waendesha Ofisi ni walinzi wa kwanza wa nyaraka na taarifa muhimu za Shirika. Alionya kuwa si sahihi kwa mtumishi kuruhusu nyaraka muhimu kuvuja kwa umma, hali ambayo imekuwa ikichangia kuibua taharuki kwa wananchi.
Aidha, Bw. Twange amesema TANESCO inathamini kwa kiwango kikubwa mchango wa kada hiyo kutokana na namna wanavyojituma kuhakikisha shughuli mbalimbali za Shirika zinafanyika kwa ufanisi, hali inayowezesha wananchi kupata huduma ya uhakika ya umeme.
“Tunawashukuru sana kwa kazi kubwa mnayoifanya. Tunaomba msichoke kuwa mabalozi wazuri wa Shirika, kusaidia kuhakikisha shughuli zetu zinaenda vizuri, na kuzingatia maadili kwa kuhakikisha mambo ya ofisi yanabaki ofisini,” amesema Bw. Twange.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala TANESCO, Bi. Margareth Mwandu, amewapongeza Waandishi Waendesha Ofisi kwa kazi nzuri wanayoifanya, akisema Shirika linawategemea kwa kiasi kikubwa katika utendaji kazi wa kila siku. Ameahidi kuwa uongozi utashughulikia changamoto zinazowakabili kwa lengo la kuboresha mazingira na ufanisi wa kazi zao.
“Pongezi za kipekee ziende kwa kada hii ya Waandishi Waendesha Ofisi. Shirika letu linawategemea sana. Ni kada muhimu mno, tunawapenda na tunatambua mchango wenu mkubwa,” amesema Bi. Mwandu.
Naye Mwenyekiti wa Waandishi Waendesha Ofisi TANESCO, Bi. Lucy Kishari, amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuwakutanisha wanachama ili kufahamiana, kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma kwa nia ya kuchochea mabadiliko chanya ndani ya Shirika.
Hata hivyo, Bi. Kishari amempongeza Mkurugenzi Mtendaji pamoja na viongozi wengine wa TANESCO kwa ushirikiano wanaowapa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Pia ameiomba TANESCO kuongeza idadi ya Waandishi Waendesha Ofisi kutokana na upungufu uliopo ndani ya Shirika.