loading...

TANESCO imetoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda La TANESCO  katika maonesho ya Biashara na Utalii yanayoendelea katika viwanja vya Usagara, Mkoani Tanga.

Akizungumza  Mei 31,2024  katika Maonesho hayo,  Meneja  wa TANESCO  Mkoa wa Tanga Mhandisi Mathias Solongo amesema kuwa Moja wapo ya elimu inayotolewa katika Banda la TANESCO ni juu ya umuhimu wa kutumia Nishati safi ya umeme kupikia, ambapo amewataka wananchi kutumia Majiko ya Umeme na kuachana na matumizi ya Kuni kwani matumizi ya Kuni hupelekea athari za kiafya kwenye macho kwa  watumiaji na uharibifu wa mazingira.

" Hapa tunatoa elimu ya matumizi Bora ya Umeme, ikiwemo matumizi ya Umeme kwenye kupikia kama Nishati safi, Kuna Majiko mbalimbali yapo hapa na mengine ni sufuria kabisa, hivi vyote tumevileta hapa kama mfano tu wa namna gani unaweza kutumia Nishati safi ya Umeme kupikia, bila kutumia Umeme mwingi na hivyo kupunguza gharama" alisema Mha.Solongo

Sambamba na hilo Mha.Solongo amewashauri wateja wa TANESCO na wananchi kwa ujumla ambao wanataka kujiunga na huduma ya Umeme  kutumia Mfumo wa Nikonekt unaowawezesha kuomba huduma ya umeme popote.

" Sasa huduma zetu zinapatikana kiganjani kwako kupitia simu Yako ya mkononi, huna haja ya kuja mpaka TANESCO, huduma zetu zipo karibu na wewe, na kama unachangamoto juu ya matumizi ya Nikonekt ukaribu sana kwenye Banda letu tutakuelekeza na utaanza kufurahia huduma hii" alisema Mha.Solongo

Naye Mkazi wa Mkwakwani Bi.Mariam Mbwana ambaye ametembelea Banda la TANESCO katika maonesho hayo amesema kuwa amepata elimu ya kutosha na kuwa Sasa ataanza kutumia Umeme kupikia kwani amekua akitumia gharama kubwa katika matumizi ya Mkaa.

" Nimeelimika sana, wajua wengi hapa tunaogopa, ukisikia jiko tu basi unajua uniti zinakwisha, kumbe rahisi tu, tena mkaa ghali zaidi" ,alisema Bi. mariam

TANESCO inashiriki maonesho ya biashara Mkoani Tanga kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu utoaji wa huduma,kutangaza Miradi ya kimkakati katika Sekta ya Nishati  inayotekelezwa pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia na hivyo inawakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Tanga na wilaya zake, kutembelea Banda la TANESCO kwenye maonesho hayo yanayoendelea mkoani humo .