loading...

Kuhusu sekta binafsi amesema, “Sekta binafsi imetutoa kimasomaso, Serikali haiwezi kufanya kila kitu, wamefanya kazi kubwa mno kwenye mafuta, gesi na hata kwenye uzalishaji umeme, wito wangu kwenu msibaki nyuma changamkieni fursa, na kwa taasisi zilizo chini ya Wizara msione sekta binafsi kama watu wajanjawajanja, tuwape kipaumbele.” Amesema Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa katika tathmini iliyozinduliwa inaonesha Sekta ya Nishati  imepiga hatua kwenye maeneo mengi ikiwemo uhakika wa upatikanaji umeme, upatikanaji na usambazaji wa mafuta kuimarika hasa baada ya Mhe. Dkt. Doto Biteko kuanza kuongoza Wizara ya Nishati.

Ameongeza kuwa, taarifa ya Benki ya Dunia kwa nchi za Dunia ya Tatu zinazofadhiliwa na Benki hiyo inaonesha kuwa Sekta ya Nishati kwa Tanzania inafanya vizuri zaidi katika nchi zote zinazoendelea na Bara la Afrika kwa ujumla na hii ni matunda ya usimamizi madhubuti wa Mhe.Dkt. Doto Biteko ambapo  eneo lililofanya vizuri zaidi ni usambazaji umeme vijijini na miradi mingine ya nishati kama JNHPP na mradi wa TAZA.

Ameongeza kuwa Benki ya Dunia imeidhinisha Dola.za Marekani milioni  300 ili ziendeleze sekta ya umeme kutokana na ufanisi huo wa Tanzania.